Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Serera (kushoto) ambaye ni msimamizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara, aktoa maelekezo wakati akisimamia uchaguzi huo.
………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
MWENYEKITI mstaafu wa jumuiya ya umoja wa vijana (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Johanes Darabe amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa Mkoa huo.
Hata hivyo, uchaguzi wa nafasi hiyo ilibidi urudiwe kutokana na mshindi Darabe kutopata zaidi ya nusu ya kura za wajumbe 522 waliohudhuria kati ya wajumbe halali 616.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera, ambaye ndiye amesimamia uchaguzi huo amesema awali Darabe alipata kura 208 na kuwashinda wagombea wenzake wawili.
Dk Serera amesema mbunge mstaafu wa Babati vijiji, Vrajlal Jituson amepata kura 183 na Mwenyekiti wa wazazi aliyemaliza muda wake Fratern Kwahhison akapata kura 131.
Dk Serera amesema uchaguzi huo ukarudiwa kwa mara ya pili kwa wagombea wawili ambapo Darabe akapata kura 290 na Jituson kura 231.
‘Wajumbe 522 walipiga kura za nafasi ya Mwenyekiti kwa mara ya kwanza na raundi ya pili wakapiga kura wajumbe 521 huku kura mbili zikiharibika,” amesema Dk Serera.
Mkuu huyo wa wilaya ya Simanjiro, pia amemtangaza Pasian Siay kuwa mjumbe wa baraza kuu la wazazi Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, baada ya kuwashinda wapinzani wake Willbroad Bayo na Stephen Manda.
Amemtangaza pia Carol Gisimoy kuwa mjumbe wa baraza kuu la UVCCM mkoa wa Manyara kupitia jumuiya ya wazazi.