Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani Makwiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo ya kinga tiba ya Matende na Mabusha Katika hafla ambayo imefanyika jijini Dar es salaam.
Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani Makwiro (kulia) akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Tabu Shaibu (kushoto) wakati wa uzinduzi wa chanjo ya kinga ya Matende na Mabusha Katika hafla ambayo imefanyika jijini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki kutoka maeneo mbalimbali wakiwa Kwenye uzinduzi huo ambao umefanyika Kwenye ukumbi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam siku ya Leo.
…………………..
NA MUSSA KHALID
Takriban wananchi Milioni moja laki mbili na elfu sabini mia nane thelathini na tatu (1,270 833) wa Wilaya ya Ilala jiji la Dar es salaam wanatarajiwa kupewa kinga tiba kwa ajili ya ugonjwa wa Matende na Mabusha.
Pia wananchi wametakiwa kuepukana na maneno ya mtaani kuhusu chanjo hiyo kwani haina madhara bali lengo lake ni kuwakinga dhidi ya maradhi hayo hivyo ni vyema wakaunga mkono zoezi hilo.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam wakati akizindua chanjo ya kinga ya Matende na Mabusha Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani Makwiro amesema kuwa maradhi hayo ya matende na mabusha siyo kwa wanaume pekee bali mpaka wanawake wanaweza kupata ugonjwa huo.
‘Chanjo hizi zitatolewa na lengo letu ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo hivyo ni vyema wote wakajitokeza kwa wingi kuonyesha ushirikikiano kwani itawasaidia kuepukana na maradhi hayo’amesema Makwiro
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Dkt Elizabeth Nyema amesema kuwa ugonjwa wa matende na Mabusha inaambukizwa na minyoo inayokaa kwenye maji damu kwenye mwili hivyo wananchi wamehamasishwa kutumia dawa hizo.
Dkt Nyema amesema kuwa watakuwa na watoa dawa hizo 478 watakao pita nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wanatoa dawa hizo zitakazowasaidia wananchi.
‘Kikubwa tunaendelea kusema kwamba madhara ya matende na mabusha yapo kuna kushindwa kufanya tendo la ndoa kwa wenye mabusha lakini kwa wale wenye matende sehemu ya mwili inaweza kuathirika na kupata vidonda mbalimbali na ugonjwa wa ngozi hivyo kinga ni bora kuliko tiba na jukumu letu tutaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kutumia neti kwani pia magonjwa hayo yanaambukizwa na mbu’amesema Dkt Nyema
Imeelezwa kuwa Chanjo hizo za matende na mabusha ambazo zitatolewa kwa siku tano tar 21 -25 mwezi huu pia zitapelekwa mpaka katika shule 110 za msingi zitafikiwa kutokana na lengo lake ni kutolewa kuanzia kwenye umri wa miaka mitano na kuendelea.