Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakaguzi wz mbolea kutoka katika mikoa 19 ya Tanzania Bara mara baada ya kufunga mafunzo yaliyofanyika kuanzia tarehe 14-17/11/2022 mkoani Morogoro. Mmoja ya wahitimu wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yaliyofanyika mkoani Morogoro Bw. Baraka Mteri kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero akikabidhiwa cheti na Mkurugenzi Mrendaji wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo Wahitimu wa mafunzo ya ukaguzi wa mbolea yaliyofanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 14-17/11/2022 wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji (waliokaa) wa mafunzo hayo kutoka Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania.
…………….
Wakaguzi wa mbolea wapya wapatao 30 kutoka mikoa 19 ya Tanzania Bara leo wamehitimu mafunzo na kupewa vyeti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt.Stephan Ngailo akifunga mafunzo hayo amesema uwepo wa wakaguzi wa mbolea nchini ni
kwa mujibu wa sheria ya mbolea Na.9 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake.
Dkt. Ngailo anewataka wakaguzi hao wa mbolea kusimamia vizuri tasnia ya mbolea kwa kufanya ukaguzi ili kuwawezesha wakulima kupata mbolea yenye ubora.
Amesena Kutokana na ukubwa wa nchi, Mamlaka itaendelea kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa mbolea ili kuwa na mkaguzi wa mbolea katika kila halmashauri nchini.”Mamlaka itahakikisha kuwa kila halmashauri nchini ina mkaguzi wa mbolea.”amesema Dkt.Ngailo.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi huyo wa TFRA Dkt. Ngailo amewataka wakaguzi wa mbolea kwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa takwimu za mahitaji na matumizi ya mbolea katika ngazi za halmashauri na amewaasa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu wa hali ya juu ikiwemo kutopokea zawadi kutoka kwa wafanyabiashara wa mbolea kwani watashindwa kusimamia kanuni sheria na miongozo iliyowekwa.
Aidha, amewataka wakaguzi hao wa mbolea kutenda haki wakati wa utekelezaji wa majukumu yao pasipo kumpendelea mtu yeyote.
Akizungumza awali, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Sagile Samweli amesema wakaguzi wa mbolea wamejengewa uwezo wa kusimamia maamuzi ya kitaalam yanayohusu ubora wa mbolea
Sagile ameongeza kuwa baada ya kupewa mafunzo hayo watahakikisha kuwa utendaji wao unazingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Mamlaka ili kuleta ufanisi unaotarajiwa.
Aidha, washiriki hao wameiomba Mamlaka iwawekee mazingira mazuri ya kutekekeza majukumu hayo mapya ya ukaguzi wa mbolea ikiwemo kuwapatia vitendea kazi ombi ambalo lilikubaliwa.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa TFRA Bi. Happiness Mbelle amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa wakulima kote nchini wanapata mbolea bora ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.
TFRA kila mwaka huandaa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea ili kuongeza idadi ya wadhibiti wa mbolea watakaoweza kufika katika maeneo yote nchini