………………………..
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
18/11/2022 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya shilingi milioni 180 ambazo zingetumiwa na Serikali iwapo ingewapeleka wagonjwa 12 wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo (Atrial Fibrillation) kutibiwa nje ya nchi.
Wagonjwa hao waliokuwa na tatizo la uzalishaji wa umeme wa moyo kwa muda mrefu uliosababisha chemba mbili za moyo kufanya kazi bila mawasiliano (Atrial Fibrillation) wametibiwa katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa na chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Cairo nchini Misri.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya siku mbili iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI Yona Gandye alisema gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa hapa nchini ni milioni 18 na nje ya nchi ni zaidi ya milioni 30 hivyo basi kuna unaafuu mkubwa wa kutibiwa hapa nchini ukilinganisha na nje ya nchi.
Mtaalamu huyo wa mfumo wa umeme wa moyo alisema hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo inaweza kusababisha damu kuganda na kupelekea mgonjwa kupata kiharusi (stroke) ama kifo cha ghafla kutokana na kiharusi.
Dkt. Gandye alisema wagonjwa wenye matatizo ya moyo ambayo ni moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), matatizo ya shinikizo la damu na mshtuko wa moyo (Heart Attack) mfumo wao wa umeme wa moyo mara nyingi unaweza kuvurugika.
“Mfumo wa umeme wa moyo ukivurugika utendaji wa kazi wa moyo hupunguza uwezo wa kufanya kazi na kuhitaji kufanyiwa marekebisho ambayo yatauwezesha moyo kuongeza ufanisi wake na kusukuma damu kwa kiwango kinachostahili,” alisema Dkt. Gandye
Dkt. Gandye alisema kupitia wataalam kutoka nchini Misri wataalam wa JKCI wamepata uwezo wa kufanya matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo kwa kujitegemea, kujenga uhusiano katika kutoa huduma hizo, pamoja na kupanua wigo na uwezo wa ndani wa kuwahudumia watanzania.
“Hapo awali huduma hii ilikuwa ikitolewa nje ya Tanzania, baada ya Serikali yetu kuanzisha taasisi hii na kufunga mtambo maalum unaoweza kusoma na kutambua matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo watanzania wameweza kupata huduma hizi hapa nchini,”.
“Moyo una uwezo wa kutengeneza mapigo yake ambayo huanza kama msisimko na kusambaa ndani ya misuli ya moyo hivyo kuufanya moyo kuweza kutanuka na kusinyaa”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema magonjwa ya moyo kuna wakati yanaweza kuwepo ndani ya mwili bila kuonesha dalili yoyote hivyo kumfanya mgonjwa kutokutafuta huduma za afya.
“Wananchi tunawahamasisha wawe wanafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kutambua matatizo mapema kwa kufanya hivyo kutarahisisha huduma kuwa nyepesi kufanyika, kupona haraka, na kupunguza madhara makubwa yanayotokana na uchelewaji wa kupata huduma kwa wakati,” alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Hospitali ya Shifa na chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Cairo nchini Misri Prof. Mervat Aboulmaaty alisema hii ni mara yao ya sita kufanya kambi hiyo na madaktari wa JKCI ambapo mafanikio makubwa yameonekana katika kutoa huduma hizo kwa wagonjwa.
Prof. Mervat alisema wamekuwa wakifanya matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuwaachia utaalam huo wataalam wa JKCI hivyo kuongeza ubingwa katika kutoa matibabu hayo hapa nchini.
“Kupitia utaalam tunaobadilishana hapa JKCI naamini Taasisi hii inaenda kuwa taasisi bora zaidi ya kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki kwani sisi ni waafrika hivyo tunapaswa kusaidiana pale tunapohitajiana,” alisema Prof. Mervat.
Naye mgonjwa aliyefanyiwa matibabu katika kambi hiyo aliwashukuru wataalam hao kwa kuokoa maisha yake na kumuondolea maumivu aliyokuwa akiyapata kutokana na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.
“Kabla ya kupatiwa matibabu nilikuwa nikipitia maumivu makali ya kifua, kizunguzungu, moyo kwenda kasi, kutetemeka pamoja na kupata ganzi maeneo ya miguuni lakini baada ya matibabu sijapata tena hizo dalili nimeamini ugonjwa wa moyo unatibika,”.
“Namshukuru Mungu na madaktari wa Taasisi hii sasa hivi naendelea vizuri, naomba utalaam huu walioupata uendelee kuwa faida kwa watu wengine wenye uhitaji wa matibabu kama niliyopatiwa mimi,” alisema mgonjwa huyo.