Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Mselem Seleman akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za Utunzaji wa Mbolea na visaidizi vyake katika mafunzo yanayofanyika mkoani Morogoro.Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi Allan Mariki akiwasilisha mada kuhusu maadili ya wakaguzi wa mbolea wakati wa mafunzo yanayofanyika mkoani MorogoroAfisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Aziz Mtambo akifafanua masuala mbalimbali kuhusu udhibiti wa mbolea wakati wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yanayofanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 14-17 /11/2022 .Afisa Udhibiti Ubora Mkuu wa TFRA Esther Kapakala akiwasilisha mada kuhusu mwongozo wa uteketezaji salama wa mbolea na visaidizi vya mbolea wakati wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yanayofanyika mkoani Morogoro.
………………………..
Wakaguzi wa mbolea nchini wametakiwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za ukaguzi wa mbolea ili kuhakikisha kuwa mbolea zinazozalishwa au kuingizwa nchini zinakuwa na ubora unaotakiwa.
Wito huo umetolewa na Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Allan Mariki, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu maadili na majukumu ya Wakaguzi wa mbolea katika mafunzo ya ukaguzi wa mbolea yanayofanyika mkoani Morogogo.
Mariki amesema kuwa wakaguzi wa mbolea wanatakiwa kufanya kazi kwa umakini na weledi mkubwa kwani maamuzi yao wakati wa ukaguzi yanagusa masuala ya afya za watu na maslahi mapana ya taifa kwa ujumla.
“Mkaguzi wa mbolea unatakiwa kuwa na kiwango cha juu sana cha maadili hususan kutenda haki kwani ukifanya maamuzi yenye upendeleo unaweza kuleta madhara katika jamii”, alisema Mariki.
Akizungumzia maadili ya wakaguzi wa mbolea
Mariki amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mbolea Na.9 ya mwaKa 2009, mkaguzi wa mbolea haruhusiwi kujihusisha na biashara ya mbolea au visaidizi vya mbolea.
Amesema mkaguzi wa mbolea anatakiwa kufanya kazi yake bila upendekeo wowote ili kutenda haki kwa wateja wote anaowahudumia wakati wa ukaguzi.
Ameongeza kuwa mkaguzi wa mbolea anatakiwa kutunza siri za taarifa anazozipata wakati wa ukaguzi na kuepuka shinikizo lolote litakaloathiri maamuzi yake wakati wa ukaguzi.
Aidha, akitoa mada wakati wa mafunzo kuhusu kanuni za utunzaji wa mbolea katika maghala, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi, Mselem Seleman amesema maghala ya mbolea na visaidizi vyake yanatakiwa kuwa safi na mahali ambapo hakuna unyevu unyevu wala hatarishi kwa mafuriko au vyanzo vya maji.
Mselemu ameeleza kuwa maghala ya mbolea yanatakiwa kuwa na kuta zisizopitisha maji, paa ambalo litazuia mwanga wa jua kuathiri ubora wa mbolea na linaloingiza hewa ya kutosha.
TFRA inatoa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea kwa maafisa ugani wapatao 30 kutoka katika mikoa 19 nchini ili kuhakikisha kuwa mbolea inayomfikia mkulima inakuwa na ubora unaokubalika .