Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Uledi Mussa akizungumza na wahariri wa habari kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya shukrani kwa mlipakodi.
Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Uledi Mussa akimsikiliza Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw.Deodatus Balile wakati wa kikao kuhusu wiki ya Shukurani kwa mlipakodi kilichofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo kulia ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo.
Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Uledi Mussa akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo.
Picha mbalimbali zikionesha baadhi ya wahariri wa habari wakiwa katika kikao hicho kuhusu wiki ya Shukurani kwa mlipakodi.
Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Uledi Mussa amesema kwa mwezi septemba mwaka huu TRA imekusanya takribani trilioni 2.3 ikilinganishwa na lengo la shilingi trilioni 2.2 makusanyo hayo bado yanaonyesha ufanisi wa asilimia 100.5 ya lengo lililowekwa na mamlaka hiyo.
Huu ni mwendelezo mzuri kutokana na serikali kukusanya jumla ya shilingi trilioni 6 katika kipindi cha mwezi Julai – septemba mwaka huu makusanyo hayo ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 99.1 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 6.1.
Bw. Uledi ameyasema hayo leo katika mkutano kati ya TRA na wahariri wa habari kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya shukrani kwa mlipakodi.
Ameongeza kuwa hii ni kutokana na juhudi za utoaji elimu kupitia vyombo vya habariambapo mamlaka hiyo imefanikiwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi hatimaye kukusanya mapato ya serikali jumla ya shilingi Trilioni 6 katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.
“Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha uliopita” Amesema Bw. Musa Uledi.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha TRA walijiwekea lengo kubwa zaidi la kukusanya mapato ya serikali ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Amewaagiza watendaji wote wa mamlaka hiyo kutotumia nguvu katika ukusanyaji mapato kwa walipa kodi badala yake kufanya mazungumzo kwa wenye malimbikizo namna gani wanaweza kulipa madeni yao bila kuathiri shughuli zao za biashara.
Nao baadhi ya wahariri katika mkutano huo wameeleza baadhi ya changamoto zinazowakumba walipa kodi nchini ikiwa ni pamoja na utozwaji wa ushuru mkubwa kwenye magari bandarini pamoja na gharama za ununuzi wa mashine za EFD ambapo wameshauri mashine hizo zigawiwe bure na TRA ili kazi yao iwe kukusanya kodi tu.