Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Fatma Mwasa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yanayofanyika mkoani Morogoro leo.Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Bi.Happiness Mbelle akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea mkoani MorogogoWashiriki wa mafunzo ya wakaguzi mbolea wakifuatilia kwa makini mada kuhusu Sheria ya Mbolea na kanuni zake iliyowasilishwa na Kaimu Meneja Huduma za Sheria Bi. Belinda Kyesi ( hayupo pichani)Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi Fatma Mwasa (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea baada ya kufungua mafunzo mkoani humo.
……………………
Morogoro.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Fatuma Mwasa amesema mbolea ni moja ya pembejeo muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji hivyo matumizi ya mbolea bora yanahitajika ili kuongeza mavuno na malighafi mbalimbali zinazotumika viwandani.
Amesema hayo mkoani Morogoro jana jumatatu Novemba 14. 2022 katika ufunguzi wa mafunzo ya maafisa ugani wanaopewa mafunzo ya kuwa wakaguzi wa mbolea
kutoka mikoa 19 ya Tanzania bara yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Amesema katika kuelekea uchumi wa viwanda, mahitaji ya malighafi ambayo kwa zaidi ya asilimia 70 ni mazao ya kilimo yataongezeka sana na kwa vile maeneo ya uzalishaji yatabaki vilevile ni wazi kwamba kuna haja ya kuongeza tija ya uzalishaji.
Aidha Mwasa amesema katika miaka mitano iliyopita Tanzania imekuwa ikitumia mbolea kati ya tani 300,000 na 500,000 za aina mbalimbali kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 30-50 ya lengo la kutumia tani milioni 1 kwa mwaka.
Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro amesema mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea kwa sasa umekuwa na umuhimu wa kipekee hasa ikizingatiwa kwamba serikali imeweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi unaotegemea viwanda.
Mwasa amewataka wakaguzi wa mbolea hao baada ya kuhitimu mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia mwongozo maalumu wa udhibiti ubora wa mbolea (Standard Operating Procedure -SOP for Fertilizer Quility Assurance Officers in Tanzania) ambao umeandaliwa mahususi kwa ajili yao.
Aidha amesema pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo wafanyabashara wachache ambao hufanya vitendo mbalimbali vya kupunguza ubora wa mbolea kwa kujua ama kutojua, jambo linalosababisha mbolea kupungua ubora wake ni vyema hatua za kisheria zikachukuliwa dhidi ya wafanyabiashara hao.
Kaimu mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Happiness Mbelle amesema TFRA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mbolea ili kuhakikisha mbolea inayopatikana nchini inatosha na inakuwa na ubora uliokusudiwa , huku ikiimarisha mawasilino kati ya Serikali na wadau wengine wa mbolea.
Mbelle amesema Mamlaka imekuwa ikifanya kaguzi kwa kushirikiana na maafisa wa halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha mbolea zilizopo sokoni zinaendelea kuwa na ubora unaotakiwa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo hiyo muhimu.
Vilevile amesema mwaka 2022/2023 Serikali imetoa Tsh.150 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya mbolea kwa wakulima na kuipa TFRA jukumu la kusimamia mpango huo.
“TFRA inasimamia mpango wa serikali wa utoaji ruzuku ili kuhakikisha kuwa unafabyika sawa na lengo kuu la serikali ya Awamu ya Sita la kupunguza makali ya bei ya mbolea kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa tija katika kilimo, kuhakikisha usalama wa chakula nchini na kuongeza malighafi kwenye viwanda”, alisema Mbelle.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kutoa mafunzo kwa maafisa ugani hao ni kutengeneza wadhibiti ubora ambao watakuwa wanafanya kaguzi katika maduka na sehemu mbalimba ili kuhakikisha mbolea inayopatikana inakuwa na ubora unaotakiwa.
Mbelle amesema mpaka sasa wadhibiti ubora 140 wamepatiwa mafuzno na wanaendelea kufanya kazi katika halmashauri mbalimbali nchini.