Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Sulumbu ( watatu Kulia) akipokea kitanda cha kujifungulia kutoka kwa Meneja wa NMB kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper( watatu Kushoto) katika hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa mbali mbali kwa kituo cha afya cha Mkinga.
Wengine ni Mganga mkuu wa wilaya ya Mkinga, Dkt Joseph Ligoha (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mkinga, Zahra Msangi (kulia)
……………………………….
Viongozi wa wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wamepongeza maono na fikra za uongozi wa Benki ya NMB nchini, kwa kusaidia sekta ya Afya hasa huduma ya mama na mtoto wilayani humo.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kukabidhi vitanda viwili na mashuka 100 kwa ajili ya kituo cha afya Mkinga vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 3.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa wilaya ya Mkinga Dkt Joseph Ligoha alisema msaada huo umetolewa kwa wakati muafaka kwa kuwa mahitaji ya vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya, katika wilaya hiyo ni mkubwa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Zahra Msangi na Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Sulumbu, waliishukuru NMB kwa msaada huo na kusema kuwa umekuja kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha suala la uzazi salama linawekewa mpango mkakati.
Aidha, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa benki hiyo ya NMB Dismas Prosper alisema benki hiyo inaishukuru na kuipongeza uongozi wa wilaya ya Mkinga kwa kuwa karibu na benki hiyo na kushirikiana nao katika mambo mbalimbali ya Maendeleo ya jamii.
Lakini pia, aiongezea kwa kusema kuwa, kwa mwaka huu wametenga kiasi cha shilingi Bilioni 2 kutoka katika asilimia moja ya mapato yake ya kila mwaka, kuzirudisha kusaidia huduma za afya na elimu kwa jamii.
Hafla hiyo iliyofanyika katika kituo cha Afya hicho, mbali na kuhudhuriwa na watumishi, wananchi wa maeneo ya jirani pia walikuwepo madiwani wakiongozwa na Makamo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Kadiri Mwaliza na diwani wa kata ya Parungu Kasera Mwajasi Bamilo.