Mkuu wa Wilaya ya kinondoni Godwin Gondwe ametoa onyo kali kwa madereva wanaondesha magari huku wakiwa wamelewa.
DC Gondwe ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na wananchi wanaoishi eneo la Wazo Hill na Madale alipotembelea eneo hilo kutokana na ajali mbaya iliyotokea jana asubuhi na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine wakijeruhiwa vibaya
” Siku za wikiendi unatokea uharibufu mkubwa wa miundombinu za barabara na maisha ya watu yanapotea hivyo wito wangu kwa madereva wasiendeshe magari wakiwa wamelewa, na tayari kamanda kashaanza ukaguzi na ameongeza askari wa kutosha kwa ajili ya ukaguzi wa magari barabarani,” DC Godwin Gondwe
Aidha Gondwe amewaomba wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu wakati Serikali inajiandaa kupanua barabara hiyo ili kuepusha ajali za mara kwa mara zinazohusishwa na magari ya kiwanda cha Twiga Cement.
DC Gondwe ameambatana na Meneja wa Tanroad ambapo amemtaka achukue maoni na maombi ya wananchi wa Wazo ya kuomba kutanuliwa kwa barabara hiyo ayapeleke Serikalini ili aweze kuingiza barabara hiyo kwenye bajeti inayokuja.
Aidha mwenyekiti wa kamati ya dharura iliyoundwa kutokana na ajali ya jana ndugu Charles Kimworo amesema kwamba baada ya kamati ya dharura kukaa na kujadiliana wanaiomba serikali kutoa tamko kwa Uongozi wa kiwanda cha Twiga Cement ili malori ya kiwanda hicho yaanze kutumia barabara mbadala ambayo ipo nyuma ya kiwanda hicho kuepusha foleni na ajali za mara kwa mara kwani barabara ya Wazo Hill kwa sasa wanatumia wananchi wengi pamoja na magari makubwa na mabasi yanayoelekea mikoa ya kaskazini.
Wajumbe wa Kamati ya Dharura wakiwa Katika picha ya pamoja.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya kikao na wananchi wa Wazo na Madale kufuatia ajali iliyotokea Jana na kusababisha kifo na majeruhi.