Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akimkabidhi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango Picha maalum ya Rais Samia Suluhu Hassan ilioandaliwa na wasanii wanaoshiriki Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani. Tarehe 11 Novemba 2022.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi na washiriki mbalimbali wa Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo wakati wa ufunguzi wa Tamasha hilo linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani leo tarehe 11 Novemba 2022. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipiga ngoma kuashiria kufunguliwa rasmi kwa Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani leo tarehe 11 Novemba 2022. (Kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa).
…………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania wote hususan wasanii wa kizazi kipya, kuepuka kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili ya taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 11 Novemba 2022 wakati akifungua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani. Ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania wakati wa utengenezaji wa maudhui ya kazi zao ili kuepukana na uvunjifu wa maadili unaojitokeza.
Makamu wa Rais amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inapaswa kushirikiana na wadau husika kuendelea kutoa elimu na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zote zinazohusiana na hakimiliki, hakishiriki, mirabaha na mikataba katika sekta ya Utamaduni na Sanaa kwa ujumla.
Pia Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha zinahifadhi, kutunza na kutangaza tamaduni za makabila kupitia utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) na kutoa nafasi kwa makabila mbalimbali hapa nchini kuonesha tamaduni zake kwenye chakula, dawa za asili, mavazi, makazi pamoja na aina ya ngoma na burudani zake. Aidha ameagiza kila mkoa kuweka utaratibu wake wa kuendeleza utamaduni wa mkoa huo kama sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa kipaumbele katika kuendelea kukitangaza Kiswahili duniani, kuhakikisha inaanzisha Kituo cha Taifa cha Sanaa cha Watoto na Vijana wenye vipaji ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa elimu, kuanza ujenzi wa Jumba Changamani la Uzalishaji wa Filamu pamoja na kuanzisha shule maalum za kukuza vipaji vya wanamichezo (sports academy).
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia itaendelea kuunga mkono wasanii hapa nchini na kuzipa kipaumbele sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili ziweze kufaidisha vijana wengi zaidi.
Kwa Upande wake Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema Wizara hiyo inalenga kuinua kiwango cha Tamasha la Sauti za Busara Zanzibar pamoja na Tamasha la Bagamoyo ili yaweze kufikia viwango vya kimataifa na kufanana na matamasha makubwa duniani.
Amesema lengo la Wizara hiyo ni kuhakikisha matamasha hayo yanakuwa na msaada wa kwa kuongeza kipato kwa wananchi, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kuitangaza nchi kimataifa.
Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linafanyika kwa siku tatu tarehe 10-12 Novemba 2022 na kushirikisha wadau mbalimbali wa Sanaa na vikundi vya Sanaa kutoka ndani na nje ya Tanzania.