Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameeleza kufurahishwa na umoja wa wadau wa habari ulioundwa kwa ajili ya kusukuma mbele mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Wabunge hao wameeleza hayo baada ya kukabidhiwa nakala za mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari ambapo wameahidi kuendelea kufanyika kazi na hatimaye kuwa na uelewa wa juu ili jambo hilo litakapofikishwa mbele yao, wapate kuishauri serikali kwa malengo mapana na manufaa ya taifa kwa ujumla.
Wabunge hao leo wamekutana pamoja na wadau wa Haki ya Kupata Habari nchini (CoRI), ili kufanya mazungumzo kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma leo Novemba 10, 2022 ambapo kuliongozwa na mmoja wa wajumbe wa CoRI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.
Katika kikao hicho, James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), pamoja na Balile waliwapitisha wabunge hao kwenye baadhi ya vipengele vya sheria ya habari ya mwaka 2016 pia mapendekezo ya wadau wa habari.
Pia wabunge hao walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo baadaye yalitolewa ufafanuzi kutoka kwa Balile na Marenga.