………………………..
Na Shamimu Nyaki – Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa asilimia 5 ya Mapato yatokanayo na Mchezo wa Kubashiri inatumika kuhudumia Timu za Taifa ikiwa ni kwa mujibu wa Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.
Naibu Waziri, Mhe. Gekul amesema hayo leo Novemba 09, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini , Mhe. David Cosato Chumi aliyeuliza kuhusu Serikali kukusanya kiasi cha asilimia 5 ya zawadi ya washindi wa kubashiri na kimechangia kiasi gani kukuza michezo.
“Kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia Septemba 2022, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi bilioni 3.4 ikiwa ni asilimia 5 ya mapato yatokanayo na Mchezo wa Kubashiri ambazo zimesaidia timu za Taifa za Tembo Worries na Serengeti Girls kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Mpira wa Miguu kwa Walemavu na Wanawake chini ya miaka 17”, amesema Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul ameongeza kuwa, fedha hizo hutumika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo na waamuzi, kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo pamoja na kukarabati miundombinu ya michezo.
Akijibu maswali ya nyongeza ya Mhe. Cosato Chumi kuhusu fedha hizo kutumika kuboresha mchezo wa riadha na mafunzo kwa ajili ya Waamuzi, Mhe. Gekul amesema kuwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Vyama vya Michezo linahakikisha linatoa mafunzo kwa waamuzi. Aidha, Shirikisho la Soka nchini (TFF) hivi karibuni limeshirikiana na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuendesha mafunzo kwa vijana 30 ambao watasaidia katika maendeleo ya michezo nchini.
Vilevile Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa timu za Taifa za Serengeti Girls na Tembo Worries kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia pamoja na Simba Queens kufuzu robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake, timu ya Simba SC kufuzu hatua ya Makundi ya Klabu Bingwa Afrika na kuitakia heri timu ya Young Africans katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Afrika leo dhidi ya timu ya Club Africain ya Tunisia.