……………………..
Na John Walter-Babati
Kuelekea mitihani ya Taifa ya kuhitimu kidato cha nne Novemba 14 hadi Desemba 1,2022, wanafunzi wamepatiwa vitendea kazi vya mtihani, Bima za Afya na taulo za kujisitiri wakati wa hedhi kwa watoto wa kike.
Zawadi hizo zimetolewa na Diwani wa kata ya Nangara Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara Samwel Barran, ikiwa ni katika jitihada za kutoa hamasa kwa wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.
Akikabidhi Msaada huo, Barran amesema furaha yake ni kuona kata hiyo inafanya vizuri kitaaluma kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na Sekondari ili wanafunzi hao wawe msaada kwa wazazi waliowalea, wao wenyewe na jamii inayowazunguka.
Mwalimu wa Taaluma wa shule ya Sekondari Nangara Yassin Jumanne amesema wameweka kambi maalum ya masomo kwa wanafunzi wa kidato cha nne ambayo imeonesha kuwa na mafanikio makubwa kwani ufaulu kwa wanafunzi hao katika mitihani wanayopewa umekuwa ukiongezeka kila siku.
Wanafunzi wa kidato cha nne wameahidi kufanya vizuri kwenye masomo yao kwa kujibu kwa usahihi yale waliyofundishwa na walimu wao kwa kipindi cha miaka minne.
Kwa upande wa Wazazi wamesema kinachosababisha baadhi ya watoto kufeli ni utoro ambao umeshindwa kukemewa na baadhi ya wazazi huku wengine wakiacha kabisa shule na kukimbilia kutumbukia kwenye kamari.