Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, Dar es Slaam (CCM), akipitia nyaraka na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wakati walipokutana jijini Dodoma.
…………………………………………
Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, Dar es Slaam (CCM), ameahidi kushirikiana na wabunge wenzake katika kuhakikisha tasnia ya habari inakuwa na sheria rafiki zinazotekelezeka.
Silaa alitoa kauli hiyo tarehe 8 Novemba 2022, wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.
TEF na CoRI walikutana na mbunge huyo ikiwa kuzungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye sheria ya habari ya waka 2016 vinavyokwaza uhuru wa habari nchini.
‘‘Mimi na wabunge wenzangu tutashirikiana. Dunia imebadilika na hatuwezi kubaki hapa tulipo,’ alisema Jerry na kuongeza ‘‘nitazungumza na wenzangu na kisha tutaona namna ya kuishauri serikali.’’
Kikao hicho nje ya viwanja vya bunge, kiliongozwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF ambapo alimweleza Jerry kwamba, sheria ya habari ya mwaka 2016 imeweka mazingira yanayokwamisha mwandishi wa habari.
‘‘Katika safari ya mabadiliko haya, tumeungana taasisi zote za habari ili kuwa na kauli moja. Tumeunganisha nguvu ili kufikia lengo ’
James Marenga, Mjumbe wa CoRI kutoka Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania alimweleza Jerry kwamba, tasnia ya habari haina tofauti na tasnia nyingine nchini katika utendaji kazi.
Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea alisema, ikiwa mawakili wanatengeneza taratibu zao na kuzifanya kuwa rejea katika kazi zao, inashindikanaje wanahabari nao wakajiwekea utaratibu wa ‘kujihukumu’ kama ilivyo tasnia nyingine?
‘‘Mimi ni mwanasheria, katika taasisi yetu tulitengeneza Cord of Conduct wenyewe na hizo ndio zinatuongozi, ni busara na wanahabari wakawa na utaratibu wao kisheria unaosimamiwa na wenyewe katika kuhakikisha maadili ya uandishi wa habari yanafuatwa,’’ alisema.