Na. Fred Kibano OR – TAMISEMI
Serikali imewataka wadau kutoa elimu kwa jamii kuelekea utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote nchini ili kujenga jamii yenye afya bora kwa maslahi ya wananchi wote .
Akifungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya, Mthibiti wa Bima za Afya nchini (TIRA) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Jijini Dodoma leo terehe 3.11.2022 Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesema suala la kuwaelimisha wananchi wote juu ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa wote ni muhimu kwani litakuwa na manufaa makubwa kwao.
Dkt. Magembe amesema timu za uhamasishaji ni lazima zikatekeleza jukumu hili la elimu kwa Umma kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na Kata hadi vijiji na vitongoji au mitaa ili kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma za afya kwa wote mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema muswada huo ukipita na kuwa sheria wananchi wote watapata huduma zote za afya katika ngazi zote kwa usawa kwa kuwa kitita cha mafao ya huduma muhimu za afya kitakuwa ni haki ya kila wanachama aliyejiunga na Mfuko huo.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Benard Konga amesema kuwa Serikali itaimarisha mfumo wa utambuzi kwa wananchi wasio na uwezo na kuweka utaratibu wa kupata huduma za matibabu kupitia Bima ya Afya kwa wote.
Ikumbukwe kuwa Serikali inaendelea kuratibu maandalizi ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2022 ambapo Muswada wa Sheria hiyo umesomwa kwa mara ya kwanza Bungeni tarehe 23 Sept, 2022 na unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika bunge la mwezi huu Novemba, 2022 lengo la Sheria hiyo inayopendekezwa likiwa ni kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.