Mkurugenzi wa Huduma za Tabiri na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Hamza Kabelwa akizungumza na wanahabari Kijiji Doeoma akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 na mwelekeo wa Utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
……………………….
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini –TMA imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa Leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Tabiri na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Hamza Kabelwa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 na mwelekeo wa Utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
Dkt Kabelwa amesema jukumu la Mamlaka hiyo kimataifa ni pamoja na kusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania.
Aidha Dkt Kabelwa amesema TMA imepanga mikakati ya kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini katika kipindi cha mwaka 2022/23.
Amesema Mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia.
“Mamlaka imeweka mikakati wa kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake” amesema Dkt Kabelwa
Kuhusu mafanikio waliyoyapa katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Dkt Hamza amesema kuwa Mamlaka hiyo iliendelea na utekelezaji wa mradi wa Rada, Vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambapo hatua mbalimbali zilifikiwa ikiwemo kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili (2) za Mbeya na Kigoma.
‘Huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ziliendelea kutolewa kwa kuzingatia mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ambalo ni ongezeko la asilimia 1’amesema Dkt Kabelwa
Vilevile Dkt Kabelwa amesema Mamlaka ilipata hati safi ya ukaguzi wa hesabu katika ukaguzi wa mwaka 2020/21 uliofanywa na wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Uboreshaji kwenye mifumo ya kihasibu ulifanyika ambapo Mamlaka ilihamia katika Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE).
Hata hivyo Mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza jukumu la kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku 5, siku 10, msimu na tahadhari ambapo usahihi wa utabiri katika kipindi husika ulikuwa asilimia 93.8 ukiwa juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika kimataifa.