Muungano Saguya Meneja habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wadaiwa sugu wa shirika hilo ambapo kampeni maalum ya kukusanya madeni itaanza hivi karibuni kulia ni Elias Msese Kaimu Mkurugenzi Usimamizi Miliki (NHC) na kushoto ni Levinico Mbilinyi Meneja wa Kukusanya madeni (NHC)
Levinico Mbilinyi Meneja wa Kukusanya madeni (NHC) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari katika mkutano huo huku Muungano Saguya Meneja habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akimsikiliza kulia ni Elias Msese Kaimu Mkurugenzi Usimamizi Miliki (NHC).
…………………………………….
Shirika la Nyumba la Taifa NHC limetangaza kampeni kabambe ya kukusanya madeni kwa Wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama ili kuhakikisha wanakusanya madeni hayo yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 26.
Shirika limekuwa likidai madeni ya kodi kwa kutumia mbinu mbalimbali ambapo juhudi hizo zimesaidia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 5 huku kiasi cha shilingi bilioni 21 zikiwa bado hazijakuswanywa.
Hayo yaneelezwa na Meneja wa habari na Uhusiano Shirika la Nyumba NHC Bw. Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya shirika hilo Upanga jijini Dar es Salaam leo jumapili 30,2022.
Amesema bado yapo pia madeni ambayo yanahitaji kufutwa na Bodi yanayofikia takriban Shilingi bilioni 6. Aidha, yapo madeni mapya yaliyojitokeza kutokana na wapangaji waliopo kwenye nyumba ambao wamelimbikiza kodi ya mwezi mmoja hadi sita. Hawa walimbikizaji ndio wanaofanya madeni ya kodi yaendelee kuongezeka.
Bw. Saguya amesema Kutokana na hali ya ukusanyaji wa madeni hayo , Shirika linawafahamisha wananchi kwamba kampeni mpya inaanza kwa ajili ya ukusanyaji wa madeni hayo.
Amefafanua kwamba kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (Active tenants) na wapangaji waliohama (Ex-tenants) wanaodaiwa malimbikizo ya kodi hadi sasa, Shirika linatoa muda wa siku sitini (60), kuanzia tarehe 01/11/2022 mpaka 30/12/2022 wahahakikishe wamelipa malimbikizo yote wanayodaiwa ili kuepuka kuchukuliwa hatua stahiki.
Ameongeza kuwa kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (Active tenants) ambao hawatalipa ndeni ya kipindi hicho, Shirika linakusudia kuvunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba na kuchukua mali zao kwa ajili ya kuuza ili kufidia madeni yao.
Aidha, kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali utekelezaji utaendelea kama notisi hizo zinavyoelekeza. Hivyo Shirika linawasihi watekeleze wajibu wao kuepuka kadhia zitakazoweza kujitokeza kwa kushindwa kufanya hivyo.
“Kwa waliokuwa wapangaji ambao wamehama na kuacha
madeni (Ex-tenants) wanayodaiwa, wanatakiwa kufika katika ofisi za Shirika zilizo karibu nao na kupewa utaratibu wa malipo ikiwemo (Control number) ili walipe,” Amesema Bw. Saguya
Amefafanua kuwa kwa wale watakaoshindwa kutekeleza ndani ya muda uliotolewa, shirika litawatangaza kwenye vyombo vya habari ili watanzania wawafahamu watu wanaokwamisha shirika na watachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
“Kitendo cha wapangaji hao kukimbia na madeni ya nyumba ni sawa na uhujumu ambao hautavumiliwa na kwamba Shirika linaenda kuwasaka popote walipo kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Shirika linashirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha kuwa wapangaji hao wanapatikana na wanalipa kodi zao,” amesema Bw. Muungano Saguya.
Amesema Shirika linawashukuru wapangaji wote wanaotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati kama mikataba ya upangaji inavyoelekeza aidha, ametoa shukurani kwa wapangaji walioitikia wito wa shirika hilo kwa kulipa madeni yao.
Shirika linapenda kuwafahamisha kuwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ni asilimia moja tu ya nyumba zote zilizopo nchini na kwamba hadi sasa kumekuwapo na maombi mapya kiasi cha 200 kila mwezi ambacho ni sawa na maombi mapya 2,400 kwa mwaka.
Maombi haya ambayo hata hivyo hayawezi kutimizwa na
Shirika kutokana na nyumba kuwa chache, yanaonyesha
watanzania wengi wanazihitaji nyumba hizi za Shirika. Kwa hiyo uhalali wa wapangaji kuendelea kuwa katika nyumba za Shirika la Nyumba utakuwepo tu kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati.
Kampeni hii ya miezi miwili itaongozwa na Kauli mbiu ya “LIPA KODI YA NYUMBA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU’’.