Mkurugenzi wa shule ya Fikiria kwanza iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha,Necta Lema akiwaasa wahitimu wa kidato cha nne katika mahafali hayo shuleni hapo.
Aliyekuwa mwenezi wa Meru Joshua Mbwana (Mwarabu)akimkabiti cheti cha kuhitimu kidato cha nne mwanafunzi wa shule ya sekondari Fikiria kwanza iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Meneja wa shule ya Fikiria kwanza ,Stephen Semfukwe akizungumza na wahitimu pamoja na wazazi katika mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
……………………..
Julieth Laizer,Arusha
Arusha.Wazazi na walezi wametakiwa kushirikiana na walimu mashuleni katika kusimamia maadili ya watoto wao ili kupata kizazi kilicho bora na salama.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na aliyekuwa Mwenezi wa Meru (Mwarabu),Joshua Mbwana wakati akizungumza katika mahafali ya kidato cha nne katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Fikiria kwanza iliyopo eneo la USA river wilayani Arumeru ambapo jumla ya wanafunzi 55 walihitimu .
Mbwana amesema kuwa, swala la kulea watoto katika maadili ni la wazazi wote kwa ujumla huku wakishirikiana na walimu ili kuweza kupata wanafunzi walio bora na wenye maadili mazuri.
Aidha amewataka wazazi kuhakikisha wanawapa watoto wao mahitaji yote wanayohitaji ili kuepukana na kujiunga na makundi yasiyofaa ambayo mwisho wa siku hukatiza ndoto zao .
“Nawaombeni sana wazazi muwe karibu na watoto wenu msiwape uhuru uliopitiliza kwani kwa kufanya hivyo mtawapoteza hakikisheni mnawalea katika maadili mazuri na yenye kupendeza ili waweze kuzifikia ndoto zao walizojiwekea.”amesema Mmbwana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule hiyo ,Necta Lema amesema kuwa,wamekuwa wakiwafundisha watoto katika maadili mazuri sambamba na kuwaandaa kuweza kujiajiri kwa kuwafundisha stadi za kazi .
Aidha amewataka wazazi wote kwa ujumla kuwajibika katika kupeleka watoto shuleni ili wapate elimu iliyo bora sambamba na kuwalipia ada kwa wakati ili waweze kutimiza malengo yao waliyojiwekea.
Aidha ameongeza kuwa,ni wakati sasa wa wazazi kujitahidi kuwalea na kuwaongoza watoto wao katika maadili mazuri ili wajiepushe na makundi mbaya huku akiwataka wahitimu kushika sana elimu kwani huo ndio uridhi pekee walioachiwa.
Naye Meneja wa shule hiyo ,Stephen Semfukwe amesema kuwa,wamekuwa wakifanya vizuri sana kitaaluma shuleni hapo ambapo wamekuwa karibu na wanafunzi katika kuhakikisha kila mmoja anafikia malengo yao kwa kuendeleza vipaji vya watoto hao.
“Katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanarudi majumbani baada ya kuhitimu nawaombeni sana wazazi mjitahidi kuwa karibu na watoto wenu sambamba na kuwafundisha kazi za mikono ili waweze kujiajiri wakiwa tangu wadogo na kuondokana na changamoto mbalimbali.”amesema Meneja .
Aidha amewataka wanafunzi hao kuongeza bidii ya kusoma zaidi na kuondokana na makundi yasiyofaa ambayo mwisho wa siku yatawaharibia maisha na kushindwa kufikia malengo yao waliyojiwekea.
Baadhi ya wahitimu shuleni hapo, Diana Mmari na Martin Francis wamesema kuwa, wanashukuru kwa namna shule hiyo ilivyowaandaa kitaaluma na katika maadili mazuri na wanaahidi kufanya vizuri katika mitihani yao na kuing’arisha shule hiyo kwa kiwango cha juu.