Na: Mwandishi Wetu, ARUSHA
Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ipo radhi kufanya mabadiliko ya sheria ya habari, na kwamba sasa umefika wakati wa kuhakikisha Taifa linapata sheria nzuri inayokidhi viwango.
Dkt. Ndumbaro alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), Jijini Arusha.
Waziri huyo alisema kuwa Serikali ina nia njema ya kutaka kuboresha Sheria hiyo ili kuwepo na mazingira bora katika Sekta ya habari hivyo aliitaka TEF na wadau wate wa habari nchini kushikamana kuendelea kuzungumzia mabadaliko hayo.
“Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.
“Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu. Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,” alisema Dk. Ndumbaro.
Akizungumzia mazingira ya sasa ndani ya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, Waziri Ndumbaro alisema, kuna kila sababu ya kutenganisha mamlaka wakati wa kupitia makosa yaliyofanywa na vyombo vya habari.
Alisisitiza kwamba, kukabidhi mamlaka ya kufungia chombo cha habari katika mikono ya mtu mmoja ni jambo hatari na haliakisi utawala wa kidemokrasia.
Aidha alitolea ufafanuzi wa kipengele hicho na kusema kuwa kinafifisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, hivyo hili ni moja ya mambo yanayopaswa kubadilishwa.
“Utatuzi wa migogoro unahitaji uwazi mkubwa. Kuna hatari kubwa katika kuweka madaraka yote kwenye chombo kimoja.
“Mimi nafahamu sheria ililenga ku-‘balance conflicting interests’ (kuweka mlinganyo kwa masilahi yanayogongana), maana serikali zote duniani huwa zinawaza kudhibiti. Alifafanua.
Katika mchakato wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari, sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa. Sheria hizi zina vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo zinahitaji kubadilishwa.