Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa – TMA Dkt Hamza Kabelwa akitangaza Utabiri wa uwepo wa upungufu wa Mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2022 mpaka Aprili 2023 Katika ofisi za Mamlaka hiyo Ubungo Plaza Leo jijini Dar es Salaam.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Tanzania -TMA imetabiri uwepo wa upungufu wa Mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2022 mpaka Aprili 2023 huku ikitoa tahadhari ya uwepo wa vipindi vifupi vya Mvua zinazoweza kuleta maafa.
Pia imewashauri wakulima katika kipindi hicho kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi zinazostahimili upungufu wa mvua yakiwemo mazao jamii ya mizizi,mikunde na mazao ya bustani.
Hayo yameelezwa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa – TMA Dkt Hamza Kabelwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa Mvua za msimu Kwa kipindi Cha Novemba 2022 Hadi Aprili 2023 ambapo amesema Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Kigoma,Tabora,Singida,Dodoma,Ruvuma,Lindi na Mtwara.
‘Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2022 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba))
unatarajiwa kuendelea kama utabiri ulivyotolewa tarehe 2 Septemba, 2022, ambapo maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani. Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari, 2023’amesema Dkt
Amesema katika Kanda ya Magharibi Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi ambapo zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2022 katika maeneo mengi na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2023. Aidha, kuna uwezekano wa mvua za nje ya msimu mwezi Mei, 2023.
Kuhusu sekta ya Afya Dkt Kabelwa amesema kuwa maeneo yanayotarajiwa kupata Mvua za chini ya wastani,upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama unaweza kujitokeza na kupelekea milipuko ya magojwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo na vikope.
Katika sekta ya Utalii, Maliasili na Wanyamapori Dkt Kabelwa amesema upungufu wa mvua unaotarajiwa katika maeneo mengi unaweza kusababisha upungufu wa maji na malisho kwa wanyamapori na kupelekea wanyamapori kuhama kwa ajili ya kutafuta maji na malisho. Hali hii inaweza kusababisha migogoro kati ya wanyamapori na binadamu na kusambaa kwa magonjwa.
‘Mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu mbalimbali katika hifadhi za wanyamapori na kujenga uelewa kwa jamii ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua inayotarajiwa. Hata hivyo, jamii inashauriwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika iwapo wanyamapori wataingia katika makazi au maeneo mbalimbali ya watu’ameendelea kusisitiza Dkt Kabelwa
Hata hivyo Mamlaka ya hiyo pia imewashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.