Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza na wadau mbaimbali wa hali ya hewa wakati alipowahimiza kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa ambazo ni chachu katika kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini alipogungua kikao cha wadau kwenye hoteli ya Tiffany jijini Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA akizungumza na wadau mbaimbali wa hali ya hewa katika kikao cha wadau kwenye hoteli ya Tiffany jijini Dar es Salaam jana.
Picha mbalimbali zikiwaonesha wadau wa hali ya hewa wakishiriki katika kikao cha majadiliano kabla ya utabiri wa mvua za msimu unaotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka
Picha ya pamoja
…………………………..
Na John Bukuku.
Taarifa za hali ya hewa ni chachu katika kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini hivyo wadau mbalimbali wanahimizwa kuzitumia taarifa za utabiri za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA, kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi,maendeleo na jamii kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akizungumza na wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili utabiri wa mvua za msimu unaotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 kwa ajili ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni mikoa ya Tabora, Kigoma Kusini,Katavi,Mbeya,Rukwa,Songwe,Njombe,Iringa,Ruvuma,Mtwara, Lindi,Dodoma, Singida na Morogoro Kusini.
“Taarifa za hali ya hewa zinalenga katika kusaidia nchi kufikia malengo ya mpango wa Taifa katika kujenga uchumi wa viwanda kwa kusaidia kupunguza athari zitokanazo na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa ili kusaidia kulinda mafanikio ya uwekezaji katika miundo mbinu ya uchukuzi ikiwemo barabara, reli na vyombo vya usafiri majini”. Amesema Dkt.Nyenzi
Ameongezea kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassankwa kuendelea kuijengea uwezo TMA, hatua ambayo imeisaidia kuboresha utabiri wa hali ya hewa na kusaidia Taifa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo upungufu wa mvua, mafuriko, joto na baridi kali pale zitakapojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi ameelezea namna serikali ilivyoendelea kuijengea uwezo Mamlaka kwa kuboresha miundo mbinu yake ambayo kwa njia moja au nyingine inasaidia kukuza uchumi wa nchi.
Dkt. Kijazi amesema mtandao wa rada upo katika hatua za mwisho ili kukamilika, huku vituo vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe vikizidi kuongezwa na mbiundombinu ya uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ikiendelea kuboreshwa, Aidha mitambo ya mawasiliano imeendelea kuboreshwa.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotels uliopo jijini Dar es Salam, Oktoba 24 ,2022.