Sylvester Hanga Mshauri Mfawidhi kutoka Taasisi ya Ushauri na Utaalam Elekezi ya Mseto akiwasilisha mada wakati wa mjadala kuhusu Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 katika kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kinachofanyika kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) akizungumza na wahariri wakati wa mjadala kuhusu Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 katika kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kinachofanyika kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam.
……………………………………………
NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Waandishi wa habari ni lazima wawe mstari wa mbele kuisemea jamii lakini ni lazima pia wahakikishe sheria zinazokizana na uhuru wa habari zinafanyiwa marekebisho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwafanya waandishi wa habari kufanya kazi yao kwa uhuru na weledi
Hayo yameelezwa na Sylvester Hanga Mshauri Mfawidhi kutoka Taasisi ya Ushauri na Utaalam Elekezi ya Mseto wakati akichangia mjadala kuhusu Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 katika kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kinachofanyika kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam
Amesema waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa ili wananchi waweze kupata habari.
Amewaomba wadau mbalimbali kushiriki katika kushawishi watunga sheria ili sheria hizo ziweze kuangaliwa na kurekebishwa kuwezesha waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wataendelea kuwa mstari wa mbele kushawishi watunga sheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili mabadiliko ya sheria zinazotatiza tasnia ya habari zifanyiwe marekebisho
“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayokabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali” amesema Deodatus Balile.
Naye mwezeshaji Tumaini Mbibo, amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.
Amesema haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia hivyo uwepo wa sheria zinazotatiza tasnia ya habari kukwamisha maendeleo hivyo vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko katika sheria hizo.