Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Sajidu Idris Mohamed (hayupo pichani) leo tarehe 21 Oktoba, 2022 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Sajidu Idris Mohamed, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo, Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Michael Sanga (mwenye shati jeusi) wakimsikiliza Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo wa Halmashauri ya Madaba (DALFO) Joseph Mrimi akieleza mwenendo wa uuzaji wa mbolea unaofanywa na wakala Mtewele aliyefikisha mbolea mjini hapo na kuanza kuuza hivi karibuni kwa kutii maelekezo ya serikali tarehe 21 Oktoba, 2022Viongozi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Sajidu Idris Mohamed (wa pili kushoto) akifuatiwa na Mkurugenzi wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo mara baada ya mazungumzo mafupi juu ya mwenendo wa usambazaji wa mbolea za ruzuku katika wilaya hiyo leo tarehe 21 Oktoba, 2022. Wa kwanza kushoto ni DALFO wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na wa kwanza kulia ni Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Michael Sanga
Mkulima Rizika Bolgias Ngonyani wa Mjini Madaba akitoka kununua mbolea aina ya SA leo tarehe 21 Oktoba, 2022 kutoka kwa wakala Mtewele General Traders and Insurance Agent wa Mkoani Njombe anayesambaza mbolea katika mikoa ya Njombe na Songea Mkulima akipewa maelekezo kutoka mtumishi wa kampuni la Mtewele General Traders and Insurance Agent alipofika ili kununua mbolea za ruzuku mjini Madaba tarehe 21 Oktoba, 2022.
…………..,…..
# Madaba nao wameanza kupata huduma hiyo
Baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuzungumza na Wakala wa usambazaji wa mbolea za ruzuku wa mkoani Njombe, Mtewele General Traders and Insurance Agent ameitika wito na kuanza kupeleka na kuuza mbolea kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba waliokuwa wakifuata huduma hiyo Songea.
Hatua hiyo imejidhihirisha leo tarehe 21 Oktoba, 2022 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo iliyolenga kujionea kiasi cha mbolea kilichopelekwa na mwitikio wa wananchi kupokea huduma hiyo.
Baada ya kujionea shehena ya mbolea katika ghala la Mtewele wilayani humo Mkurugenzi wa TFRA Dkt. Ngailo alimwagiza Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (DALFO) wa Halmashauri hiyo, Joseph Mrimi, Dkt. Ngailo alimtaka kuzungumza na wananchi wa eneo lake na kuwatoa hofu kuwa mbolea hazitoshelezi na kwamba ruzuku inaukomo.
“Muwaambie wananchi mbolea ipo yakutosheleza mahitaji kwa maimu wote wa kilimo hivyo wasiwe na wasiwasi, mbolea haitaisha wala mpango wa ruzuku hautaisha hivyo wasiwe na wasiwasi” alikazia Dkt. Ngailo.
Aliongeza kusema, kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akihutubia wananchi kwa nyakati tofauti tofauti anasema mbolea za ruzuku zitatolewa kwa msimu wote wa kilimo wa mwaka 2022/2023 kuanzia mwezi Agosti 2022 alipotoa tamko mpaka tatehe 30 June 2023 mwaka wa fedha wa Serikali utakapokuwa unakwisha.
Akijibu swali la mwandishi wa habari wa Azam TV Mkoa wa Njombe, Emmanuel Kalemba aliyetaka kujua juhudi zinazochukuliwa na mamlaka katika kuhakikisha mbolea inafikishwa karibu na maeneo wakulima walipo, Dkt. Ngailo alieleza kuwa changamoto hiyo imeanza kutatuliwa kwa kuongeza mawakala katika maeneo mbalimbali yaliyobainika kuwa na changamoto hiyo.
Aliyataja maeneo yalitafutiwa ufumbuzi kuwa ni pamoja na Madaba ambapo wakulima wameanza kununua mbolea leo tarehe 21 Oktoba, 2022.
Amesema, kwa upande wa Ludewa Kata zilizosogezewa huduma ni pamoja na Madilu, Madope, Lupanga, Lubonde, Amani, Mlangali, Lugalawa, Mundindi na Milo na maeneo mengine yenye changamoto ufumbuzi unaendelea kutafutwa.
Akifafanua kuhusu upatikanaji wa stika kwa ajili ya kuuza mbolea kwa mujibu wa taratibu za utekelezaji wa mpango wa ruzuku, Mkurugenzi Dkt. Ngailo amesema awali kulikuwa na mtoa huduma mmoja lakini kwa sasa TFRA inazalisha QR code na makampuni yenye uwezo wa kudurufu yanaruhusiwa kufanya hivyo na hivyo changamoto ya stika kwa sasa imekwisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Sajidu Idris Mohamed alisema ukanda anaousimamia ni ukanda wa kilimo hivyo mahitaji ya mbolea ni makubwa.
Aidha, Sajidu Idris alipongeza juhudi za serikali na mamlaka kwa ujumla za kuhakikisha maeneo yenye changamoto yanafikishiwa mbolea na hivyo kuwasaidia wakulima kupunguza gharama ya kufuata mbolea mbali na maeneo wanayolima.