Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerad Mweli akifafanua jambo wakati wa kikao cha wafanyabiashara wa mbolea kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa mbolea wakiwa katika kikao cha pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Andrew Massawe kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya kilimo, Jijini Dar es Salaam.
………………………….
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe amewataka wafanya biashara wote wa mbolea nchini kuongeza kasi ya kusambaza pembejeo hiyo muhimu ili iwafikie wakulima kwa wakati.
Bwana Massawe amesema hayo jana tarehe 19.10.2022 jijini Dar es Salaam alipokutana na waagizaji wa mbolea kwa lengo la kutathmini kwa pamoja utekelezaji wa mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa msimu wa Kilimo wa 2022/2023.
Katibu Mkuu huyo amesema hali ya usambazaji wa mbolea katika maeneo mengi ya pembezoni mwa nchi hairidhishi ambapo tayari msimu wa kilimo umeshaanza.
“Suala la kufikisha mbolea kwa wakulima kwa wakati linaendana na msimu, hivyo ni muhimu kwa makampuni na mawakala wa mbolea kufanya kila linalowezekana kuwafikia wakulima kwa wakati”, Alisema Bw. Massawe.
Massawe aliyataja maeneo ambayo yana mawakala wachache wa mbolea kuwa ni Mara, Kagera, Geita , Nkasi, Kalambo, Meatu, Itilima, Busega, Maswa, Momba, Kiteto na Babati.
Aliongeza kuwa maeneo mengine yenye mawakala wachache ni Nyasa, Tunduru, Lindi, Pwani, Siha, Hai, Mwanga, Same Moshi, Longido, Monduli, Simanjiro Arumeru , Makete, Ludewa, Mbarali, Chunya na Shinyanga.
Kufuatia uhaba wa wasamvazaji wa mbolea katika maeneo hayo Massawe ameyataka makampuni ya mbolea kuhakikisha wanafikisha huduma katika maeneo hayo ndani ya wiki moja ili kuwawezesha wakulima waweze kupanda mazao yao kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya makampuni ya mbolea, mwakilishi wa Kampuni ya Yara, Januari Fabian aliiomba serikali kuwawezesha kupata usafiri wa bei nafuu ili waweze kufikisha mbolea kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Fabian alisema kuwa gharama za usafiri wa kufikisha mbolea katika maeneo ya pembezoni mwa nchi imekuwa ni kubwa kwao hivyo wanaiomba selikali kuwasaidia.
Makampuni ya mbolea pia wameiomba serikali kuwasaidia kupata maghala ya kuhifadhia mbolea katika maeneo yaliyo karibu na wakulima.
Akijibu kuhusu maombi ya makampuni hayo Naibu Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Gerad Mweli amesema serikali imechukua hoja hizo na itazifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima kwa wakati.