Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi –sekta Uchukuzi Atupele Mwakibete akizungumza wakati akizindua Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo imefanyika leo jijini Dar es salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt Matiko Mturi (aliyesimama) akitaja majukumu ya bodi ambayo imezinduliwa leo jijini Dar es salaam na aliyekaa kulia kwake ni Naibu Katibu Kuu sekta ya Ujenzi Rudovick Nduhiye.
Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt Fatma Mohamed akizungumza baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo ambayo imefanyika leo jijini Dar es salaam.
Picha ya Pamoja Menejimenti ya Baraza la Taifa la ujenzi (NCC) pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi –sekta Uchukuzi Atupele Mwakibete (katikati) Naibu Katibu Kuu sekta ya Ujenzi Rudovick Nduhiye (wa pili kushoto),Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt Fatma Mohamed (wa pili kulia).(picha na Mussa Khalid)
…………………….
NA MUSSA KHALID
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi –sekta Uchukuzi Atupele Mwakibete ameitaka bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kutoa miongozo ya thamani halisi ya miundombinu ya Barabara ili kuokoa pesa za serikali zinazopotea kutokana na kukosa miongozo sahihi.
Naibu Waziri Mwakibete ameeleza hayo Jijini Dar Es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambapo amesema kuwa kwa sasa serikali imekuwa na kilio cha miradi yake kuwa na gharama kubwa ambayo imetokana na kukosa mwongozo sahihi wa ujenzi.
Naibu Waziri Mwakibete ameitaka Bodi hiyo kutunga sheria ya majenzi,kuja na miongozo ya ujenzi,kuja na kanuni za ujenzi pamoja na kuifanya tathini ya ujenzi iheshimike ili kuweza kubadili mtazamo wa wadau kuhusu bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi(NCC).
Aidha,Mwakibete ameikata Bodi hiyo kuhakikisha wanazingatia sheria za utumishi wa umma na kuacha kufanya vitendo vya udanganyifu pamoja na vitendo vya rushwa bali wawe mfano katika kutekeleza miradi mbalimbali.
Naibu Waziri Mwakibete amewakumbusha kuwa matarajio ya serikali ni pamoja na kupata mabadiliko makubwa katika taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa kwa mujibu wa mipango ya kila mwaka.
‘Nakuagiza Naibu Katibu Mkuu ujenzi kwa niaba ya Katibu Mkuu mabadiliko haya watakayokuwawanaleta kwenu muweze kuyasimamia na kuyaratibu na kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili yalete tija iliyokusudiwa’amesema Naibu Waziri Mwakibete
Awali akitoa taarifa kuhusiana na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC),Afisa Mtendaji Mkuu wa baraza hilo Dkt Matiko Mturi ameyataja majukumu yake kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya kukua kwa sekta ya ujenzi nchini.
Dkt Mturi ameeleza kuwa jukumu lingine ni kufanya utafiti na kuratibu kufanyika kwa utafiti utakawezesha maendeleo katika sekta ya ujenzi lakini pia kuwezesha migogoro inayotokea katika sekta ya ujenzi hasa kwenye miradi ya ujenzi kupata utatuzi wa haraka na kuleta tija.
‘Pamoja na kuwa na mafanikio tumekuwa na changamoto chache ikiwemo ya uhaba wa wataalamu wa kada za uhandisi,za ukadiriaji majenzi na kada za ubunifu majengo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt Fatma Mohamed amemuahidi Naibu Waziri kuwa watafanya kazi kwa bidii na ueledi ili kutimiza majukumu yao ipasavyo ili kuleta mabadiliko katika sekta ya ujenzi nchini.