Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa akijibu hoja za wabunge akiwemo Mbunge wa Songea Vijijini Jenista Mhagama na Mbunge wa Madaba Josephy Mhagama juu ya utekelezaji wa mpango wa ruzuku na kueleza juhudi zinazofanywa na Serikali za kuhakikisha mbolea inafikishwa alipo mkulima. Ametoa kauli yake akizungumza na hadhira iliyoshiriki uzinduzi wa hospitali ya Wilaya ya Madaba uliofanyika tarehe 19 Oktoba, 2022 Mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (mwenye kofia nyeupe) akifuatilia tukio la uzinduzi wa hospitali ya Wilaya ya Madaba uliofanywa na Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 19 Oktoba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Songea Vijijini Jenista Mhagama akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa hospitali ya wilaya ya madaba uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo pichani) tarehe 19 Oktoba 2022
…………………
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka wakulima nchini kujipanga kulima kwa tija na kubainisha serikali imeweka mipango mahususi kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo ya mbolea kwa wakati na kwa bei himilivu.
Amewahakikishia wakulima wanaofanya shughuli zao za kilimo mbali na maeneo ya mijini kuwa, makampuni ya mbolea yameelekezwa kuhakikisha wanakuwa na mawakala wenye uwezo wa kusambaza mbolea katika maeneo waliyopo wakulima ili kuwapunguzia mzigo wa kwenda mwendo mrefu kufuata bidhaa hiyo.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo leo, tarehe 19 Oktoba, 2022 alipokuwa akiihutubia hadhira iliyoshiriki hafla ya uzinduzi wa Hospitali ya Wilaya ya Madaba kwa lengo la kuwapunguzia wananchi kadhia ya kwenda mwendo mrefu ili kupata huduma za afya.
Amesema, mahitaji ya mbolea kwa mkoa wa Ruvuma ni tani elfu sitini na saba (67000) na kubainisha kuwa mpaka sasa tani 2467 zimesambazwa kwa wakulima na kwenye maghala kuna kiasi cha tani elfu moja na laki tano kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa mkoa huo
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema zaidi ya tani elfu hamsini zinashushwa bandarini huku tani elfu ishirini na tatu zikitarajiwa kushushwa ifikapo Novemba tarehe 22, 2023 na baadaye kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini Ruvuma ikiwemo.
Majaliwa ameendelea kusema mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula na kueleza mbolea kutofika Ruvuma ni kukaribisha njaa nchini jambo ambalo halikubaliki.
“Niwahakikishie wananchi wa Madaba na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuwa mbolea zitaletwa jipangeni tunawategemea sana kwa ajili ya kupata chakula” Majaliwa amesisitiza.
Aidha, Majaliwa ametaja kampuni za uingizaji wa mbolea nchini zinazosambaza pembejeo ya mbolea katika mkoa wa Ruvuma kuwa ni pamoja na Mohamed interprises LTD, YARA Tanzania LTD, OCP, na Premier na kubainisha kuwa mazungumzo yamefanyika kuhakikisha wanakuwa na mawakala wa kutosha watakaofikisha mbolea karibu na wakulima.
Kwa upande wao Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama na Mbunge wa Madaba Josephy Mhagama walieleza changamoto ya mawakala kupatikana mbali na maeneo yenye wakulima jambo lililotolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu Majaliwa.