Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Jumamosi, 15 Oktoba, 2022 alizindua kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220/33 kutoka Bulyanuhlu hadi Mpomvu Geita.
Hapo awali Mkoa wa geita wenye wilaya tano ulikuwa ukipata umeme mdogo kutokea Shinyanga wa Megawati 4. Kutokana na ukuaji wa uchumi, umeme huo ulikuwa ni kikwazo kwa shughuli za kiuchumi hususani katika sekta ya madini.
Uwepo wa kituo hiki utaufanya mkoa wa Geita kupata umeme wa Megawati 90 ambapo mahitaji ya Geita kwa sasa ni Megawati 18.
Kukamilika kwa kituo hiki kunaifanya Geita pia kuanza kupata umeme wa kutosha kwa shughuli za kiuchumi na za kijamii.
Pamoja na kuondoa tatizo la umeme mdogo ambapo awali maeneo ya mkoa wa Geita ikiwemo Chato na Sengerema yalikuwa yakipata changamoto hiyo na kushindwa kufanya shughuli zake za kiuchumi kwa ufanisi, TANESCO ilikuwa inashindwa kuwapatia umeme wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini kama vile Geita Gold Mines (GGM), Geita Gold Refinery na StamiGold.
Kwa sasa TANESCO inaweza kuwapelekea umeme wateja wakubwa na wadogo na tayari Shirika limesaini mkataba na Mgodi mkubwa wa Geita Gold Mines (GGM) na kukamilisha njia itakayopeleka umeme kwenye mgodi huu mkubwa.
Hatua hii itaongeza mapato kwa Shirika kwa kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa mwezi na kupunguza gharama za uendeshaji kwa GGM kwa shilingi bilioni 4 kwa mwaka. Migodi midogo itakayonufaika ni pamoja na maeneo ya Nyarugusu, Rwamgasa, Nyakangwe, Msasa, Iparamasa, Katente, Nyakafuru, Shenda na Mwamakiliga.
Vilevile Mheshimiwa Rais amezindua mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Mpovu Geita ambapo mradi huo wenye sehemu tatu ambazo ni Njia ya kusafirishia umeme kutoka Bulyanhulu mpaka Geita yenye uwezo wa kilovoti 220 za umeme.
Mitambo umba za kupoza umeme zenye uwezo wa kupitisha megawati 90 na Usambazaji umeme katika Wilaya ya Geita.Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais amewasihi wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waendelee kuchapa kazi kwa bidi na wala wasivunjike moyo.
“Niwaombe wafanyakazi msivunjike moyo, najua huenda kinachopatikana ni tofauti na matokeo ya kazi mnayoifanya, lakini huko mbele mambo yakikaa sawa tutagawana kitakachopatikana.
’’Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande amesema kuwa uzinduzi wa kituo hiki cha Mpomvu utaondoa changamoto iliyokuwepo ya umeme mdogo pamoja na kushindwa kuwapelekea umeme wa uhakika wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini.
Gharama zilizotumika kutekeleza Mradi huo ni jumla ya dola za kimarekani milioni 23 (Shilingi bilioni 50.63 fedha za kitanzania) ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa dola milioni 3, BADEA na OFID (The Opec Fund for International Developement) dola za kimarekani milioni kumi kila mmoja.