DAR ES SALAAM.
Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kukamilika kwa Udahili kwa Awamu ya Nne na ya mwisho kwa ngazi ya Shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2022/2023.
Akizungumza katika taarifa yake aliyoitoa leo Oktoba 15, 2022 kwa maandishi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema kuwa majina ya waombaji waliodahiliwa katika awamu ya nne yatatangazwa na vyuo husika.
“Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika awamu ya nne na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili wao katika awamu zilizopita wanahimizwa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo tarehe 15 hadi 24 Oktoba 2022 kwa kutumia namba maalum ya siri inayotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumiwa wakati wa kuomba udahili”
“Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya siri ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika” amesema Prof. Kihampa.
Aidha uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili. Orodha ya majina ya waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja imewekwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).
Waombaji udahili wa Shahada ya kwanza wanakumbushwa kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika. Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.