Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani SACP Wilbrod Mutafungwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam kuhusu kuhusu wanaotumia magari yaliyobandikwa na kutumia namba ambazo hazijatolewa na (TRA),pamoja na na wanaofanya matumizi ya ving’ora,vimulimuli na taa za kubadilisha rangi kwenye magari yao wawapo barabarani.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani SACP Wilbrod Mutafungwa akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Kamanda wa ambao wamehudhuria wakati Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani SACP Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
…………………..
NA MUSSA KHALID
Jeshi la Polisi Kikosi Cha usalama Barabarani nchini limetoa tahadhari kwa madereva na wamiliki wa magari yaliyobandikwa na kutumia namba ambazo hazijatolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au Taasisi za Kiserikali ambazo zimepewa jukumu hilo kisheria kuacha mara moja vitendo hivyo kwani ni kinyume na sheria.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani SACP Wilbrod Mutafungwa ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam ambapo amesema wamebaini kuna magari barabarani ambayo yanatumia namba ambazo hazijatolewa na Mamlaka husika hivyo ni vyema wakaziondoa kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Aidha Kamanda Mutafungwa amesema vitendo wanavyofanya madereva na wamiliki wa magari hayo ni kinyume cha sheria ya Usalama barabarani sura ya 168 ya Mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.
‘Katika kifungu cha 14 (2) kama kinavyosomeka pamoja na Tangazo la serikali na,177 la mwaka 2001 linalohusu usajili wa magari.Kwa mujibu wa sheria hiyo hakuna mtu anayeruhusiwa kuweka namba za usajili katika gari au tela zisizo halisi na zisizotambulikwa kwa msajili wa magari’amesema SACP Mutafungwa
Katika Hatua nyingine Kamanda Mutafungwa amewataka madereva pindi wawapo barabarani kuepukana na matumizi ya ving’ora,vimulimuli na taa za kubadilisha rangi kwenye magari yao kwani matumizi hayo yamekuwa yakisababisha usumbufu usio wa lazima kwa watumiaji wengine wa barabara.
Kamanda Mutafungwa amewakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani magari yanayoweza kutumia Ving’ora kwa dharula ni magari ya kubeba wagonjwa,magari ya zimamoto na magari ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Ameendelea kusema kuwa magari mengine yaliyopatiwa kibali na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi na kutangazwa kwenye gazeti la serikali ni magari ya viongozi wakuu wa kitaifa.
‘Tunawataka madereva na wamiliki wa magari,pikipiki na bajaji kuondoa vifaa hivyo mara moja kabla ya hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao’Ametoa wito Kamanda Mutafungwa
Jeshi hilo limesema litaendelea na oparesheni mbalimbali ya kukabiliana na makosa ya usalama barabarani kwa kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria madereva wa vyombo vya moto waaotenda makosa ya usalama barabarani.