Na Mwandishi wetu,
Geita
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania,TMDA kanda ya Ziwa Magharibi,Geita imewataka watanzania kuendelea kuwa makini na matumizi ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi kwa kuhakikisha kuwa zinakidhi ubora wa matumizi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TMDA wa Kanda hiyo Dkt Edgar Mahundi alipokuwa akizungumza na waadishi wa habari katika banda la mamlaka hiyo kwenye maonyesho ya 5 ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema lengo la mamlaka ya dawa na vifaa tiba kanda ya ziwa magharibi,Geita ni kushiriki katika maonyesho hayo na kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya matumizi sahihi ya dawa,vifaa tiba na vitendanishi ili wananchi hao wawe na uelewa pindi wanapokwenda kununua dawa hizo.
Ameongeza kuwa wapo wafanyabishara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za dawa na vifaa tiba ambavyo havikidhi ubora unaohitajika,zilizokwisha matumizi (Expire)pamoja na dawa feki hivyo mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi sambamba na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa na vifaa tiba kukamata na kuteketeza dawa na vifaa tiba hivyo ambavyo vimekwisha muda wa matumizi.
Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 mamlaka hiyo kanda ya ziwa magharibi,Geita imekamata dawa mbalimbali zilizokwisha muda wa matumizi,zilizo chini ya kiwango,ambazo hazijasajiliwa na feki pamoja na kukamata dawa za kusisimua misuli na kuongeza nguvu za kiume ambazo pia ni feki.
Amesema dawa hizo hata katika maelezo ya kiwanda kinachotengeneza mamlaka ilifuatilia na kubaini kiwanda hicho hakipo wala kutambulika sehemu yoyote duniani na vijana wanaozitumia wanaweza kuja kupata matatizo makubwa baadaye kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Hata hivyo amewataka vijana wa kiume kuachana na matumizi ya dawa hizo za kuongeza nguvu za kiume kwani zina madhara makubwa yanayoweza pia kuchangia kuharibu mfumo wa uzazi.
Kuhusu kukamatwa kwa dawa za kuzuia kubeba ujauzito maarufu kama P2 ambazo ni feki na ambazo hazijasajiliwa hapa nchini Dkt. Mahundi amesema kuwa walibaini dawa hizo zikiuzwa katika maduka ya kawaida ya dawa kinyume na utaratibu dawa hizo (zilizokidhi ubora)zinatakiwa zitolewe na madaktari katika vituo vya afya na si maduka ya dawa na tayari wamekwisha chukua hatua huku akiwataka wanawake wanaotumia dawa hizo bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya waache mara moja kwani zinaweza kuchangia baadaye kushindwa kupata ujauzito endapo zitatumiwa bila kufuata ushauri wa wataalam wa afya.
Aidha mamlaka hiyo ya dawa na vifaa tiba imesema kuwa itaendelea na operesheni zake katika maeneo mbalimbali kukagua kama dawa na vifaa tiba vinavyouzwa madukani vimekidhi viwango vya ubora unaohitajika hapa nchini na itachukua hatua kwa wafanyabishara watakaobainika kuuza dawa hizo,sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya dawa,vifaa tiba na vitindanishi.