*Ni yale yaliyofutwa na Rais Samia baada wawekezaji kushindwa kuyaendeleza
*Madiwani wajanja wajanja watakiwa kuacha kutafuna fedha za halmashauri
**********************
Na Sulemani Jongo, Kilosa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amevunja ukimya baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuamua kuyafuta mashamba makubwa 14 yenye ekari 23,016 katika halmshauri za wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro na kisha kuyagawa kwa wananchi.
Akizungumza wakati akizindua msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Morogoro, jana wilayani Kilosa, Shaka alisema ufutaji wa mashamba hayo haukufanywa kwa bahati mbaya au kwa kubahatisha bali ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi tumezungumza vizuri sana, ukisoma Ibara ya 74 tumezungumza vizuri namna ya kuhuisha na kuboresha matumizi bora ya ardhi, lakini tumezungumza namna ya kufuta mashamba ambayo kwa muda mrefu kuna watu walijimilikisha na wakayatelekeza.
“Lakini mashamba ambayo wajanja wajanja waliamua kuyachukua kwa njia moja au nyingine ili kukwamisha shughuli za maendeleo ziweze kufanyika. Bahati nzuri nimewahi kuwa Katibu wa CCM katika Mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha miaka miwili.
“Nilipofika kwenye mkoa huu kwa kipindi cha miezi sita sikukaa ofisini nilikuwa nakuja na kurudi Kilosa asubuhi na jioni. Kazi moja kubwa ambayo niilifanya kwa ustadi mkubwa ni kupokea malalamiko ya ardhi, nadhani kwenye Mkoa wa Morogoro na hasa Kilosa ilikuwa inaongoza kwa malalamiko ya ardhi. Kesi kubwa za wilaya hii wako watu wamejimilikisha mashamba na hayaendelezwi,” alisema.
Aliongeza kuwa wako wajanja wamechukua mashamba ya wenzao lakini hakuna kinachofanyika, lakini kesi kubwa ya Kilosa ilikuwa ni namna ambavyo hakukua na mpango bora wa matumizi ya ardhi ndani ya wilaya hiyo.
“Kwa mtazamo wangu kwa sababu sisi tulifanya kazi kubwa sana na tulifanya kazi ngumu kweli kweli, kwa maoni yangu viongozi mlioko kwenye mkoa huu mmeanza vizuri,” alisema.
Shaka alisema Rais Samia tangu ameingia madarakani ameweka mkazo na msisitizo katika kilimo na ndio maana wote ni mashahidi kwani ameongeza bajeti ya kilimo kwa kiasi kubwa kutoka Sh. bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi sh. bilioni 954 mwaka 2022/2023.
“Hiyo haijapata kutokea tangu tumepata uhuru kwenye bajeti ya kilimo yenye fedha nyingi kama hii. Tafsiri yake tunakwenda kutafsiri kwa vitendo kilimo ndio uti wa mgongo lakini kilimo ndio mkombozi kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Alitoa rai kwa viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanawawezesha vijana kwenye maeneo ya kilimo na utaratibu mzuri hasa kwa kuzingatia shamba ambalo wamepewa wananchi lina hati moja, ndani yake vijana wamewagawa na kuwapanga vizuri .“Rai yangu vijana hawa lazima wawezeshwe kwa mitaji, vijana lazima wawekewe utaratibu mzuri wa kusimamiwa na tuhakikishe wanaendelea sio wanarudi nyuma,” alisema.
Alisema ni vema madiwani na viongozi wengine kwenye ngazi ya halmashauri kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha zinafika kwa walengwa.
RC MOROGORO
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amefuta mashamba makubwa 14 yenye ukubwa wa ekari 23,016 katika Halmashauri za Mvomero na Kilosa ili yagawiwe kwa wananchi jambo ambalo limeelezwa ni heshima kubwa kwa wananchi.
Mwasa alisema mashamba hayo yameanza kugawanywa kwa wananchi kwa mfumo wa Block Farming ili kuongeza ufanisi zaidi.
“Pia wakulima watapewa elimu ya kuunda AMCOS ili kurahisisha usimamizi.Aidha Serikali katika kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji imetoa ruzuku kwa mbolea za kupandia na kukuzia, mbolea ya UREA ,DAP zinauzwa kwa bei ya ruzuku ya Sh.70,000 kwa mfuko wa kilo 50.Bei bila ruzuku ingekuwa Sh.130,000,” alisema.