Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini –TFRA Dkt Stephan Ngailo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam akitoa taarifa ya kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Mbolea Duniani yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 13 Mwaka huu.
.…………………….
NA MUSSA KHALID
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini -TFRA imesema itaendelea kuimarisha tasnia ya Mbolea nchini ikiwemo kuweka Mazingira wezeshi yanayovutia na kukuza uwekezaji katika tasnia hiyo na sekta ya kilimo Ili kuongeza tija Katika uzalishaji wa mazao mbalimbali Nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt Stephan Ngailo wakati akitoa taarifa ya kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Mbolea Duniani yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 13 Mwaka huu katika Mkoa wa Songwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
Dkt Ngailo amesema lengo la maadhimisho hayo ni kupanua wigo zaidi wa kuelezea Masuala mbalimbali katika tasnia ya Mbolea yakiwemo mafanikio ya tasnia hiyo pamoja na kutoa elimu kwa wadau wa mbolea hususani wakulima na wafanyabiashara wa mbolea kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ya ruzuku kwa kilimo chenye tija.
“Juhudi za serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Katika kuthamini mchango wa sekta ya Kilimo ambapo katika msimu wa 2022/2023 serikali imetenga kiasi Cha Sh 150 Bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa utoaji wa Ruzuku ya Mbolea Kwa wakulima Ili kuwapunguzia makali ya bei ya Mbolea”amesema Dkt Ngailo
Aidha Dkt Ngailo amesema Mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha mifumo ya Udhibiti wa Mbolea Ili kuhakikisha wakulima wanapata Mbolea Bora wakati wote.
Mkurugenzi Huyo ameeleza kuwa tangu Mwaka 2016/2017 Hadi septemba Mwaka huu,JUMLA ya Mbolea zilizosajiliwa zilikuwa 447 na hivyo kuongezeka Kwa Mbolea zilizosajiliwa kufaa kwake Katika urutubishaji wa udongo.
Kuhusu mafanikio Dkt Ngailo amesema TFRA imefanikiwa kuimarisha Mfumo wa utoaji huduma za mbolea ambapo kwa sasa huduma hutolewa kwa kutumia Mfumo wa Kimtandao wa Mbolea (Fertilizer Information System-FIS ) ambao ulianza Machi mosi Mwaka 2021.
“Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya viwanda vya kuzalisha Mbolea nchini kwani kabla ya Mwaka 2016,Tanzania ilikuwa na viwanda vya Mbolea vinne na hapakuwepo na kiwanda hata kimoja Cha visaidizi vya Mbolea hivyo kutokana na uhamasishaji na utashi wa kisiasa wa serikali Sasa kuna viwanda kumi na nane ambavyo huzalisha aina mbalimbali za mbolea na visaidizi vyake”ameendelea kusisitiza Dkt Ngailo
Hata hivyo Dkt Ngailo amewataka wakulima wote nchini kuendelea kujitokeza kwa wingi kujisajili kwa ajili kunufaika na mbolea ya ruzuku ambayo serikali inaendelea kutoa kwa msimu huu.