Baadhi ya makasisi wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA wilayani Tunduru wakiwa kwenye maandamano kabla ya Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa kwanza wa Kanisa hilo Noel Mbawala(hayupo pichani).
Kanisa ya Upendo wa Kristo Masihi KIUMA kama linavyoonekana.
Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Kiuma Noel Mbawala kulia,akimsikiliza Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt Donald Mtetemela(hayupo pichani)wakati wa ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mbawala kuwa Askofu wa kwanza wa kanisa la Upendo Kristo Masihi KIUMA wilayani Tunduru.
Viongozi wa Taasisi ya Kiuma na familia ya Profesa Diechmann kutoka nchini Ujerumani wakifuatilia ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa kwanza wa Kanisa la Upendo Kristo Masihi KIUMA wilayani Tunduru.
Mhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa kwa niaba ya makanisa la jumuiya ya Kikikristo Tanzania(CCT)akizungumza na waumini wa kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUM na baadhi ya wageni waliohudhiria Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa kwanza wa kanisa hilo Noel Mbawala(hayupo pichani).
Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt Donald Mtetemela akizungumza wakati wa Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA wilayani Tunduru.
Wanafamilia ya ProfesaDiechmann kutoka Nchini UJerumani ambao ni wafadhili wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA,wakimpongeza Askofu wa kwanza wa Kanisa hilo Noel Mbawala kulia baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu.
Askofu wa kwanza wa kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA wilayani Tunduru Noel Mbawala akizungumza na waumini na wageni watu waliohudhuria Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Kanisa hilo.
Mwakilishi wa Shirika la Neno na Tendo(Word&Deed Mission) kutoka Ujerumani ambao ni wafadhili wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA lililopo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Susanna Diechmann akitoa salamu za shirika la familia wakati wa Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa Kanisa hilo Noel Mbawala.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro akizungumza wakati wa kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA Wilayani humo Noel Mbawala.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro katikati aliyevaa suti akiwa katika picha ya pamoja na makasisi na maaskofu wa kanisa la Anglikana Tanzania baada ya kumalizika kwa Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu wa kwanza wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi KIUMA Noel Mbawala(hayupo pichani).
Picha zote na Muhidin Amri,
…………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
ASKOFU Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt Donald Mtetemela,amewataka viongozi wa Dini nchini kujiepusha na kauli na vitendo vitakavyopandikiza chuki na uchochezi kwa waumini wao dhidi ya Serikali na dini nyingine.
Askofu Mtetemela ametoa kauli hiyo jana,wakati wa Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Kasisi Noel Mbawala kuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi(KIUMA)lililopo kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilaya ya Tunduru.
Ibada hiyo imeongozwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimba Mndolwa kwa niaba ya Makanisa ya Jumuiya ya Kikiristo Tanzania (CCT) baada ya kanisa hilo kujiunga rasmi na jumuiya hiyo.
Aidha Dkt Mtetemela,amewataka viongozi wa dini hapa nchini,kushirikiana na kuheshimu mamlaka za serikali ili kuendelea kutunza amani na mshikamano uliopo badala ya kuwa chanzo cha mfarakano na migogoro isiyokuwa na manufaa kati ya waumini,serikali na jamii kwa ujumla.
“ili mtu uwe kiongozi nzuri ni muhimu sana kushirikiana na serikali iliyopo madarakani,kuwa na maono,dira ,na mahusiano kwa waumini wako na wale wa dini nyingine,kiongozi asiye na mahusiano na maono kamwe hawezi kufanikiwa katika nafasi yake”alisisitiza Askofu Mtetemela.
Amewakumbusha viongozi na waumini kuwa,katika mifarakano na uhasama wowote ndani ya kanisa hakuna atakayeibuka mshindi bali wote watakuwa watu tulioshindwa.
Dkt Mtetemela amesisitiza,kiongozi nzuri siyo anayefanya maamuzi bila kuwashirikisha wengine,bali ni mwenye kushirikisha wenzake, na waumini wa dini nyingine na kulisaidia kanisa kuibua vyanzo na miradi mingi ya maendeleo.
Amewaasa viongozi kuacha tabia ya kung’ang’ania madaraka ili kuepusha migogoro na migongano inayoweza kuwagawa waumini wao na kuhatarisha uhai na usalama wa kanisa.
“mara kadhaa tumeshuhudia migogoro na mapigano kwenye makanisa watu wakigombea madaraka na mali,nawakumbusha viongozi kufuata misingi na taratibu ziliowekwa na ikiwamo kuachia madaraka pindi muda unapokoma”alisisitiza Dkt Mtetemela.
Dkt Mtetemela,amewataka viongozi wa dini na Serikali kuwa na hofu ya Mungu, kauli nzuri kwa watu walio chini yao,kujiepusha na wizi na kujilimbikizia mali kwani kufanya hivyo itapelekea kutoamini na kuheshimika kwa waumini wao na jamii.
Amewaomba waumini wa kanisa hilo,kushirikiana na viongozi wao na kuzika(kusahau)tofauti za nyuma na kulisaidia kanisa,kutunza mali ili ziweze kuwafikia wahitaji wenye matatizo na shida mbalimbali.
Katika hatua nyingine Dkt Mtetemela,amempongeza mwasisi wa Kanisa hilo Dkt Matomoro Matomora na familia ya Profesa Diechmann ya Ujerumani ambayo imetumia sehemu ya mapato yake kuanzisha kanisa na taasisi ya Kiuma ambayo imekuwa na mchango mkubwa kupunguza tatizo la umaskini,afya na elimu kwa Watanzania.
Mwakilishi wa familia ya Profesa Diechmann ambayo ndiyo mfadhili wa kanisa hilo Susanna Diechamann alisema,familia inafarijika kuona misaada wanayotoa kwa kanisa na la Upendo Kristo Masihi na taasisi ya Kiuma inatumika vizuri na kuhaidi kuendelea kushirikiana katika kutoa huduma kwa kanisa na huduma za kijamii.
Amempongeza Askofu Mbawala kwa kusimikwa kuwa kiongozi wa Kanisa hilo ambapo alieleza kuwa,hatia hiyo inalifanya kanisa la Upendo wa Kristo Masihi sasa kuwa na uongozi baada ya kuondoka kwa mwasisi wa kwanza Dkt Matomora Matomora.
Amemtaka Askofu Mbawala na watumishi wengine wa Taasisi ya Kiuma,kuhakikisha fedha zote zinazoletwa zinatumika kama ilivyokusudiwa ili kuimarisha huduma za kanisa na za kijamii kama elimu na afya.
Kwa upande wake Askofu wa kanisa la Upendo wa Kristo Masihi(KIUMA)Askofu Noel Mbawala,amehaidi kuwatumikia vyema waumini wa kanisa hilo,kujifunza,kusimamia misingi na malengo ya kanisa,kushirikiana na waumini na Serikali iliyopo madarakani.
Kwa mujibu wa Askofu Mbawala ni kwamba, umoja na ushirikiano kati ya kanisa,waumini na serikali ndiyo utakao msaidia katika kuendesha na kuongoza taasisi ya KIUMA ambayo tangu ilipoanzishwa imekuwa na mchango mkubwa kwa watu wa mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla.
Aidha,ameipongeza serikali kwa kuimarisha na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwamo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbambabay-Mbinga-Songea hadi Tunduru.
Alisema,kuimarika kwa huduma za kijamii hasa barabara hiyo imesaidia sana hata watumishi wanaoletwa kufanya kazi katika wilaya ya Tunduru kutofikiria kuhama kutokana na mazingira mazuri yaliyopo kwa sasa.
Hata hivyo,ameiomba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia watumishi hasa wa sekta ya afya ili waweze kuongeza nguvu na kupunguza changamo ya uhaba wa wataalam kwenye Hospitali ya KIUMA.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amehaidi kuwa,serikali itaendelea kushirikiana na kuzitegemea taasisi za dini kujenga misingi imara ili kudumisha amani miongoni mwa Watanzania.
Alisema,serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa watu wake kuabudu dini wanayoamini kwa sababu ni moja kati ya haki za msingi za kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na itafanya kila iwezalo kuhakikisha uhuru huo unaheshimiwa.
Alisema,uhuru wa kuabudu ni nyenzo muhimu iliyowezesha Tanzania kuwa mfano wa kuigwa kote Ulimwenguni ambapo amehaidi serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini zote ili kuhakikisha uhuru wa kuabudu hauchezewi na mtu au kikundi chochote.