*Shaka asema mpango utakapokamilika wananchi waiunge mkono serikali*
*Apongeza NMB kuhamasisha jamii katika maendeleo*
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kugusa maisha ya wananchi kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kuwa utawasaidia wengi kupata huduma za matibabu kwa uhakika.
Aidha, kimeipongeza benki ya NMB kwa kuendelea kushiriki masuala ya kijamii yakiwemo yanayoihusu afya ambayo ni muhimu kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka baada ya kukaribishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, atoe salamu za Chama katika mbio zilizoandaliwa na NMB kwa ajili ya kuchangia matibabu ya wagonjwa wa Fistula, waliopo katika Hospitali ya CCBRT jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kutambua matibabu haya yana gharama kubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 83 kifungu (e) inaelekeza katika kipindi cha miaka mitano, tutahakikisha kwamba tunaweza mazingira rafiki ya upatikanaji wa huduma hizi za afya. Nichukue fursa hii kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi kumpongeza kwa dhati kabisa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali anayoiongoza kwa kuweka mpango madhubuti ya bima ya afya kwa wananchi wote.
Alisema wakati NMB wakishiriki jitihada katika kuimarisha sekta ya afya kwa kukusanya sh. milioni 600, Rais Samia ameshaweka miundombinu ya kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma hizo kupitia bima ya afya ili kupunguza makali ya upatikanaji wa huduma hizi.
“Ndugu zangu nataka niwahakikishie kuwa hamtajutia uamuzi wa kuiamini serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi niwaahidi kwamba Chama kitaendelea kuziunga mkono taasisi zote zinazounga mkono juhudi za maendeleo. Kazi ni moja na kazi inaendelea bila ya kurudi nyuma.
Alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 83, imeelekeza kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano, serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi itaimarisha huduma za afya kwa wananchi, ikiwa sambamba na ujenzi wa vituo vya afya, upatikanaji wa vifaa tiba na kuimarisha miundombinu ya maeneo ya kutolea huduma za afya, NMB hongereni sana kwa kuunga mkono jitihada za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
AIPONGEZA NMB
Shaka aliipongeza benki ya NMB kwa namna ambavyo imeweka mipango na utaratibu wa kuishirikisha jamii katika masuala mbalimbali ya kijamii.
“Kitendo cha kuandaa tukio hili kutafuta fedha kwa ajili ya changamoto inayowakabili baadhi ya kinamama nchini ni hatua kubwa na ya kupongeza sana.
“Fistula imekuwa ikiwakosesha kujiamini na imekuwa ikiwakosesha furaha baadhi ya akinamama, huu leo ni ukombozi wa kurudisha heshima, kurudisha utu na kurudisha kujiamini kwa baadhi ya akinamama ambao wanapambana na changamoto hii.