Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Sahili Gezarura akizungumza na klabu ya Malaria katika shule ya sekondari Kasimba
Jengo la wagonjwa wa nje katika kituo cha afya cha MwangazaViongozi wa mbio za mwenge wakikagua daraja la Kigamboni katika Manispaa ya Mpanda.
………………………….
Na Zillipa Joseph Katavi
Jumla ya miradi 10 katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano imefikiwa na mwenge wa uhuru 2022.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa daraja la Kigamboni lililo jengwa kupitia Fedha za tozo ya mafuta kiasi cha Tsh. Milioni 500 ambapo kabla ya Daraja hilo kujengwa wananchi wa kata ya Shanwe, Misunkumilo na Makanyagio walikuwa wanapata adha ya kufuata huduma mjini hasa nyakatiza mvua.
Miradi mingine ni ujenzi wa tenki la maji kijiji cha Kakese, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha afya Mwangaza lililoghalimu kiasi cha Tsh. Milioni 150.
Aidha miradi mingine iliyokaguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Sahili Gezarura ni pamoja na uzinduzi klabu ya kupinga ugonjwa wa malaria ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Kasimba, klabu ya lishe ya wanafunzi wa shule ya sekondari St. Mary’s na ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari Rungwa.
Miradi mingine ni pamoja na kiwanda kidogo cha kukamua alizeti kinachoendeshwa na vijana wa kikundi cha Kusakizya wanaofanyia shughuli zao katika karakana ya SIDO manispaa ya Mpanda.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Sahili Geraruma pia amegawa vyandarua kwa kinamama wajawazito na wenye watoto pamoja na watu wenye ulemavu katika kupiga vita ugonjwa wa malaria.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa kufanya vizuri katika matumizi ya Fedha na utekelezaji wa miradi licha ya kuwepo kwa mapungufu machache kwenye baadhi ya miradi ambayo tayari ameagiza yafanyiwe marekebisho.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph ameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 kuhusu kufuatilia mapungufu yaliyojitokeza.
‘Tunamshukuru sana Rais wetu mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii’ alisema.
Naye Mbunge wa jimbo la Mpanda mjini Sebastian Kapufi amesema serikali itaendelea kuwajali wananchi wake kwa kuwafikishia huduma mbalimbali.