Na Zillipa Joseph, Katavi
Uwepo wa viwanda vidogo vidogo vya wajasiriamali vya kukamua mafuta ya alizeti katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kumesaidia ongezeko la upatikanaji wa mafuta hayo na hivyo kupelekea kupungua kwa bei ya mafuta ya kula.
Kwa kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi juni mwaka huu Bei ya mafuta ya kupikia hususan alizeti kwa mkoa wa Katavi ilikuwa ni kati ya shilingi elfu tisa hadi kumi na mbili kwa lita moja, tofauti na sasa ambapo mafuta ya alizeti yanauzamwa kwa shilingi elfu tano hadi sita kwa lita moja.
Hayo yamebainika wakati mwenge wa Uhuru kitaifa ulipotembelea kikundi cha Vijana cha Kusakizya kinachofanya shughuli za kukamua mafuta katika eneo la karakana ya Shirika la viwanda vidogo vidogo(SIDO).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kiwandani hapo kikundi hicho kinajiendesha kwa mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 30
Aidha wameeleza kuwa wana uwezo wa kuzalisha tani saba kwa siku na tayari wamefungua duka maeneo ya soko kuu la Mpanda kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa bwana Sahili Geraruma amewataka viongozi wa Manispaa kuendelea kutoa mikopo kutokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani.
Bwana Geraruma pia amewakumbusha wataalamu wa Halmashauri wakiwemo maafisa maendeleo ya jamii kuhakikisha taratibu zote za kupata mikopo zinafuatwa.