Wakufunzi wa Vyuo 10 vya Ualimu kutoka Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi wamekutana na Kamati ya kitaifa ya uboreshaji Mitaala na kutoa maoni na mapendekezo yao juu ya uboreshaji wa Mitaala Leo tarehe 24/09/2022
Wakufunzi hao kutoka vyuo vya Ualimu vya Tabora, Kinampanda, Bustani, Mpwapwa, Shinyanga, Tarime,Bunda, Murutunguru, Katoke na Butimba wamekutana na kamati hiyo kwa lengo la kutoa maoni na mapendekezo juu ya uboreshaji wa Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Ualimu.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi uliopo jengo la Osha Jijini Dodoma Mwenyekiti wa Kamati Prof.Maboko aliwasilisha mapendekezo ya muundo wa Ualimu na mabadiliko yaliyopendekezwa.
Aidha Prof.Maboko amesema mtaala ni mali ya jamii hivyo ni lazima kupata maoni na mapendekezo kwa jamii ili kupata Mitaala itakayokidhi matakwa ya jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu ya Ualimu Bwana.Huruma Mageni ameishukuru kamati kwa kuweza kuwashirikisha Wakufunzi hao, na kusisitiza kuwa kada ya Ualimu ni lazima iwe na mabadiliko makubwa kwa sababu walimu ndio walengwa wakuu wa Elimu yetu hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba aliwasilisha wasilisho juu ya taarifa ya matokeo muhimu kutoka kwenye taarifa ya uchambuzi wa maoni ya wadau kuhusu Elimu ya ualimu.
Dkt.Komba amesema kuwa mabadiliko makubwa ya mtaala ni ya awamu ya sita yatakayogusa mfumo mzima wa elimu na yenye lengo la kumjengea muhitimu ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa.
Pia aliwashukuru Wakufunzi hao kwa kuitikia wito wa kuja kutoa maoni na kuwahakikishia kuwa kamati teule ni sikivu imeyapokea maoni na mapendekezo na itaenda kuyachakata ili kupata Mitaala yenye kukidhi malengo ya Taifa.
Maoni na maboresho mbalimbali yametolewa na kupokelewa na kamati ya uboreshaji mitaala iliyoteuliwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ambayo inaongozwa na mwenyekiti Prof.Makenya Maboko.