Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amefungua kikao kazi cha kujadili Usimamizi na Uendeshaji wa SACCOS kilichofanyika katika Ukumbi wa Ngome Holding Jijini Dar Es Salaam leo tarehe 23/09/2022.
Akifungua kikao hicho, Mrajis alieleza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeandaa Taarifa ya Utendaji wa SACCOS kwa mwaka 2021 (The SACCOS Annual Performance Report 2021) yenye lengo la kupima utendaji wa shughuli za SACCOS kwa mwaka 2021. Taarifa hiyo itakuwa inaandaliwa kila mwaka.
Dkt. Ndiege amesema mkakati huu utasaidia SACCOS kuweka mipango yenye ufanisi yanayopimika katika utekelezaji wa shughuli za Chama ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“SACCOS zinaendeshwa kwa kuzingatia Mifumo iliyowekwa na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na Miongozo mingine inayotolewa kwa Maendeleo ya SACCOS nchini, na hii inapelekea Vyama kuendelea kusajiliwa na kukua kwa kasi zaidi,” amesema Dkt. Ndiege.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendelea kusimamia na kuhamasisha Maendeleo ya Ushirika ili kuondoa taswira mbaya iliyojengeka kwa jamii kuwa Ushirika haufai kwa kuweka mifumo thabiti na kuonesha manufaa ya Vyama vya Ushirika kupitia mafanikio na masuala mazuri yanayofanyika ndani ya Sekta ya Ushirika.
“Ushirika husaidia wanachama kuinua uchumi wao na kujiendeleza kwa masuala ya Maendeleo kama vile kusomesha, kujenga na kuanzisha biashara,” alisema Dkt. Ndiege.
Vilevile Mrajis alisema kuwa ni wakati wa SACCOS zote nchini kuanzisha Mfuko wa Kinga za Akiba na Amana. Mfuko huo utakuwa na faida kwa wanachama wote na endapo SACCOS ikishindwa kujiendesha Mfuko huo utasaidia kuwalipa wanachama fedha ambazo walizoweka kwenye SACCOS. Hivyo aliwataka washiriki kujadiliana na kutoa maoni juu ya uanzishwaji wa Mfuko huo.
Pia, amewataka Viongozi wa SACCOS kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyotolewa na Mrajis ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Dkt. Ndiege aliwasisitiza Wanaushirika kuwa wakifanya kazi kwa kufuata miongozo na kwa uwazi Vyama vitafanikiwa katika nyanja zote na kujibu mahitaji ya wanachama wao.
Aidha, Mrajis amezitaka SACCOS zote na Wadau wa Maendeleo ya Ushirikia kuendelea *kununua Hisa katika Benki ya Ushirika ya KCBL itakayopelekea kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika (NBCT)* ambayo itasaidia kuimarisha Sekta ya Ushirika ikiwemo Ushirika wa SACCOS.