…………………..,….
Mradi wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira, ujulikanao kama “SHARPP” umeleta mafaniko makubwa katika kuboresha utawala bora na kuleta uwazi katika usimamizi wa maliasili, uhifadhi wa ushoroba wa wanyamapori mkoani Mbeya.
Aidha, mradi huo umeimarisha usimamizi bora wa misitu na maeneo mengine yenye umuhimu wa kibaiolojia pamoja na ushiriki wa wananchi katika kuhifadhi na kufaidika na raslimali za maliasili zinazowazunguka.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana, Mkoani Mbeya alipokuwa akifunga rasmi mradi huo ambao umekuwa ukitekelezwa kwa miaka minane iliyopita tangu 2014 kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Misaada la Watu wa Marekani – USAID na Shirika la Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WCS).
“Programu ya Uhifadhi wa Nyanda za Juu Kusini na Ruaha-Katavi (SHARPP) ilianzishwa mwaka 2014 katika ukanda huu wa nyanda za juu kusini mwa Tanzania kwa kutambua hitaji muhimu la kuimarisha ulinzi wa maliasili, makazi ya wanyamapori na mfumo wa ikolojia wa moja ya eneo muhimu kwa uhifadhi wa baioanuai katika Afrika Mashariki”. Alisema Mhe Balozi Dkt. Chana
Waziri Balozi Dkt Chana, ameongeza kuwa, matumizi ya ardhi yasiyozingatia mipango bora ya ardhi kama vile, kulisha mifugo na watu kuweka makazi sehemu zisizoruhusiwa, ukataji miti hovyo kwa ajili ya mbao, mizinga ya kienyeji, uzalishaji wa mkaa usio endelevu, uchomaji moto na uchimbaji madini huchangia katika uharibifu wa mazingira na bioanuai katika maeneo yaliyohifadhiwa.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, inauthamini uhifadhi wa wanyamapori na Mazingira kama njia mojawapo na bora ya kuinua uchumi na maendeleo ya watu wake” Aliongeza Mhe. Balozi Dkt Chana
Licha ya kuwapongeza walewote waliofanikisha mradi huo, Mhe Balozi Dkt. Chana amesema, Serikali imejipanga kushirikiana na wadau wote kupitia Taasisi zake, wakiwemo Wananchi, washirika wa maendeleo, na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali katika kuwekeza kwenye uhifadhi wa maliasili nchini.