Mratibu wa Mtandao wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa pamoja na Mkurugenzi wa UTPC, Bw. Keneth Weston Simbaya wakati alipotembelea ofisi za Mtandao zilizopo Mikocheni B, Jijini Dar es Salaam mapema leo.
……………….
Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu umefurahi kupokea ugeni wa Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), na Mjumbe wa bodi ya THRDC aliyemaliza muda wake mwaka jana, Bw. Keneth Weston Simbaya.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa Afisa Habari THRDC imesema Simbaya ametembelea ofisi za Mtandao wa THRDC kwa mara ya kwanza leo tangu kuchaguliwa kuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo mapema mwezi Julai 2022, na kukutana kwa mazungumzo na mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa.
Kikao hicho kimejadili mambo mbali mbali ya mashirikiano baina ya Mtandao na UTPC katika kukuza na kuendeleza tasnia ya Habari nchini, hususani kuwaendeleza kwa kuwajengea uwezo waandishi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi huku wakizingatia misingi ya tasnia, sheria na pamoja na Haki za Binadamu.
Tangu kuanzishwa kwake, THRDC imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na tasnia ya Habari, hasa katika kuwajengea uwezo waandishi wa Habari katika maswala mbali mbali ya haki za binadamu, pamoja na Msaada wa dharura pindi mwandishi anapopatwa na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa majukumu yake.