Daraja la Ibumba lenye urefu wa mita 60 linalounganisha wilaya za Sikonge na Urambo Mkoani Tabora ambalo linajengwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika Kijiji cha Ibumba kata ya Ibumba, wilayani Sikonge Mkoani Tabora kwa gharama ya sh bil 1,9 likiwa katika hatua za mwishoni kukamili.
……………………………………
Na Allan Kitwe,
TaboraWAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) wamefanikiwa kujenga daraja kubwa lenye urefu wa mita 60 katika Kijiji cha Ibumba kata ya Ibumba,
Wilayani Sikonge Mkoani Tabora ili kumaliza kilio cha muda mrefu cha wakazi wa wilaya 2 za Urambo na Kaliua.
Ujenzi wa daraja hilo linalounganisha wilaya hizo 2 sasa umefikia asilimia 96 na unatarajia kugharimu kiasi cha sh bil 1.9 hadi kukamilika hivyo kuokoa roho za wananchi ambazo zimekuwa zikipotea kwa kusombwa na maji katika eneo hilo.
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa gharama ya sh bil 1.9 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu hivyo kuwezesha watumiaji barabara hiyo kuepuka usumbufu waliokuwa wanapata.
Akizungumza na gazeti hili baada ya kutembelea mradi huo jana, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatus Mativila alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha ili kujengwa daraja hilo.
Alisema daraja hilo ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya hizo na maeneo jirani kwani wataweza kuondokana na adha kubwa waliyokuwa wanapata kipindi cha masika hali iliyopelekea kushindwa kusafirisha mazao yao kutoka shambani.
Aliongeza kuwa umbali wa kutoka Sikonge kwenda Urambo kupitia barabara hiyo ni km 70 tu ikilinganishwa na umbali wa kutokea Sikonge kwenda Urambo kupitia Tabora mjini wa km 120, hivyo daraja hilo linalounganisha Mto Wala na Kasisi litarahisisha shughuli za kiuchumi.
Mhandisi Mativila alipongeza Kampuni ya Nyegezi J.J Construction inayojenga daraja hilo kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwataka kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo mapema iwezekanavyo.
Aidha alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kutunza miundombinu ya mradi huo ili udumu kwa muda mrefu huku akibainisha kuwa serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja hilo ili kuwaondolea kero waliyokuwa wanapata.
Mtendaji wa Kijiji cha Ibumba kilichoko katika kata hiyo Bartholomeo Athanas alishukuru serikali kuwajengea daraja la kisasa katika mto huo kwani mvua ikinyesha mto huo ulikuwa haupitiki na watu wengi walishapoteza maisha.
“Serikali imesikia kilio chetu, tunashukuru sana, pia tunawapongeza TANROADS kwa kusimamia vizuri ujenzi wa mradi huu, tunaomba Mkandarasi aongeze bidii ili likamilike haraka tuanze kulitumia kabla mvua hazijaanza kunyesha’, alisema.
Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo Emanuel Mokaka alieleza kuwa zaidi ya watu 10 walishapoteza maisha katika eneo hilo kwa kusombwa na maji na akinamama 2 wajawazito walishindwa kuvuka wakajifungulia kando ya mto huo.
Alibainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo akashukuru serikali kwa kutenga kiasi hicho cha sh bil 1.9 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, aliomba wakazi wa kata hiyo kulitunza vizuri.
Matolo Shija mkazi wa kata hiyo alisimulia jinsi alivyosombwa na maji katika mto huo ambapo aliparamia mti uliokuwa katika mto huo kabla ya kuokolewa na waendesha mitumbwi waliokuwa wakiwatoza sh elfu tano tano kila kichwa.