Na Englibert Kayombo – WAF, Bungeni Dodoma.
Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo Bungeni Jijini Dodoma akiwa anajibu maswali ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalim kuhusu ujenzi wa Hospitali hiyo.
Aidha Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma katika Hospitali ya sasa ambapo majengo yake ni chakavu.
Hata hivyo Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Sekta ya Afya kwa kuajili watumishi wapya na kutoa fursa za elimu kwenye fani za mbalimbali za Afya ikiwemo taaluma za kibingwa.
Akijibu swali kuhusu mpango wa Serikali kupeleka madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Dkt Mollel amesema Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari watano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, ambao ni madaktari wawili wanasomea upasuaji, daktari mmoja anasomea upasuaji wa Mifupa (Orthopaedics), Daktari mmoja anasomea magonjwa ya dharula (EMD) na daktari mmoja anasomea kinywa, sikio na koo (ENT).
Dkt. Mollel amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa watano wa fani za Afya ya mama na uzazi (Obsy/gyn) wawili, magonjwa ya watoto (paediatric) wawili pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) mmoja.