Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam (kushoto) pamoja na Wajumbe kutoka vyama vyote viwili katika kikao kilichofanyika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akimpatia zawadi ya kinyago chenye maana ya umoja Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam (kushoto) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akiwa kwenye picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya CCM na Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV), kupitia udugu na urafiki wa kihistoria wa vyama hivyo viwili.
Ndugu Chongolo amesisitiza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Mambo ya Nje wa CPV, Ndugu Troung Quang Hoai Nam, leo tarehe 19 Septemba, 2022 katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Chongolo ameeleza umuhimu wa kuboresha na kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya CCM na CPV ambayo yanalenga katika kupanua wigo wa ushirikiano katika maeneo mbalimbali yakiwepo uwekezaji katika kilimo, biashara na pia mafunzo na kubadilishana uzoefu wa kiuongozi kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote viwili.
Katika mazungumzo hayo, Ndugu Chongolo amesisitiza namna ambavyo Tanzania imeweka mkazo katika kilimo cha umwagiliaji kuwa mojawapo ya mikakati ya kukabili na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, ambapo ushirikiano katika eneo hilo utatengeneza fursa za kuajiri watu wengi, ambapo serikali ya awamu ya sita imeweka fedha nyingi katika eneo hilo ili kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji wenye tija na kukuza uchumi.
Ameongeza kuwa, ushirikiano katika masuala hayo, ni mojawapo ya maeneo yatakayoongeza chachu ya udugu na uhusiano mwema wenye tija kwa maendeleo ya uchumi baina ya pande hizo mbili.
Aidha, kwa upande wake Ndugu Troung pamoja na mambo mengine kwa niaba ya CPV ametilia mkazo wa kudumisha, kukuza na kuendeleza zaidi ushirikiano katika kuzalisha ajira kupitia uwekezaji katika Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji kwani CPV na Viet Nam imefanikiwa sana katika kilimo hicho, kutokana na kuwa na miundombinu iliyojengwa miaka mingi nyuma.