1. Bandari ya Dar es Salaam (DSM) imeendelea kutumia vyema faida kijiografia katika kuhudumia shehena mbalimbali za mzigo za nchi jirani hususan nchi ya DRC. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha unaoanzia mwezi Julai 2021 hadi Juni 2022, shehena ya mzigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam imeongeza kwa asilimia 49 ukilinganisha na mwaka 2020/2021.
2. Kuongezeka kwa shehena ya DRC kumechagizwa na hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na wadau wa Sekta ya Uchukuzi nchini.
3. Hatua ambazo zimechagiza mafanikio ya sasa ya Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia shehena ya DRC zinajumuisha: –
a. Tozo nafuu za kibandari zinazotozwa na Bandari ya DSM ukilinganisha na bandari shindani.
b. Nyongeza ya muda huru wa hifadhi wa shehena bandarini (free storage period) kwa shehena ya DRC kutoka siku kumi na nne (14) hadi siku thelathini (30) iliyotolewa na Serikali mnamo mwaka 2018 ili kupunguza gharama za kuhifadhi shehena bandarini wakati ikisubiri kusafirishwa.
c. Kutoa punguzo na unafuu wa tozo za bandari (concessionary tariff) kwa wateja wote kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vya kimasoko na kisera.
d. Kupunguza idadi ya mizani ya kupima uzito wa malori kutoka mizani tisa (9) hadi mizani mitatu (3) kutoka bandarini hadi mpakani.
e. Kusogeza karibu huduma kwa wateja wa DRC kwa kufungua Ofisi ya TPA jijini Lubumbashi.
f. Kukamilika kwa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam kupitia mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP), mradi ulioongeza uwezo wa kimiundombinu pamoja na ufanisi wa bandari ya DSM.
4. Hatua hizo zimefanikiwa kuifanya bandari yetu kuendelea kuwa shindani katika uhudumiaji wa shehena za nchi jirani hususan kwa nchi ya DRC ambapo Bandari ya DSM ndio kinara wa uhudumiaji wa shehena hiyo hadi sasa.
5. Ili kuendelea kuifanya Bandari ya DSM kuwa shindani pamoja na kuongeza ufanisi wa uhudumiaji wa shehena ya DRC, Serikali kwa kushirikiana na TPA imeendelea kufanya yafuatayo:-
a. Kutenga jumla ya hekta kumi (10) katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala, Mkoa wa Pwani pamoja na hekta kumi (10) katika eneo la Katosho, Kigoma kwa ajili kupatiwa Serikali ya DRC kwa matumizi ya ujenzi wa Bandari Kavu zitakazohudumia shehena za mzigo wa DRC.
b. Kutanua wigo wa huduma kwa wateja kwa kufungua ofisi nyingine katika eneo la Kolwezi kabla ya Mwezi Novemba 2022 ili kuwasogezea kwa ukaribu zaidi huduma za kibandari wafanyabiashara wa DRC waliopo eneo hilo.
c. Kutekeleza Mpango Kabambe wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na DRC wa kuimarisha miundombinu ya bandari, barabara na reli katika ushoroba wa kati (Dar-Kigoma-Kalemie-Lubumbashi. Mkatati huu umelenga kufungua ushoroba mpya ili kuhudumia soko la DRC pasipo kulazimika kupitia Zambia. Utekelezaji wa mpango husika utajumuisha: –
i. Ujenzi na ukarabati wa reli upande wa DRC unaounganisha maeneo ya Kalemie, Kabalo-Kabongo, Kamina pamoja na Lubumbashi.
ii. Ukarabati wa Bandari ya Kalemie pamoja na kununua vifaa vya kuhudumia shehena.
iii. Kuendeleza bandari kavu za Katosho (Tanzania) na Kalemie (DRC).
iv. Kujenga meli ya abiria na mizigopamoja kukarabati meli ya mafuta MT Sangara
d. Serikali ya Tanzania kuendelea kushirikisha na kuziwezesha Sekta binafsi katika kufanya uwekezaji wa usafirishaji Ziwa Tanganyika kwa kuruhusu kuleta meli kubwa zaidi kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa shehena na abiria kati ya Tanzania na DRC.
e. TPA kuendelea kufanya maboresho ya huduma kwa meli na shehena katika bandari ya DSM na Bandari ya Kigoma ili kupunguza muda wa meli kukaa bandarini pamoja na kuongeza shehena zaidi inayohudumiwa kupitia bandari hizo.
6. Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na Bandari ya DSM na hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa, Serikali ya Tanzania imeendelea kuwa tayari kuchukua hatua nyingine zozote zitakazoonekana zinafaa wakati wowote ili kuhakikisha shehena ya DRC inahudumiwa kwa ufanisi zaidi na kwa gharama nafuu kupitia Bandari zake.