Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni, jijini Dodoma.
………………………….
Na. Rahma Taratibu (SJMC)
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kujadiliana na wafanyabiashara wenye malimbikizo ya kodi ili kuwapa unafuu wa kulipa malimbikizo ya kodi kwa awamu bila kuathiri ukwasi, mwenendo na uendeshaji wa biashara.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asha Abdullah Juma kuhusu hatua zinazochukuliwa kwa walipa kodi walioshindwa kulipa na kuwa na malimbikizo makubwa lakini wapo tayari kulipa kutokana na agizo la Mhe. Rais.
Mhe. Chande alisema kuwa majadiliano hayo yanayoendelea na wafanyabiashara ni katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
“Sheria ya Usimamizi wa Mapato, Sura 438 Kifungu cha 70 na Kanuni zake kinampa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusamehe adhabu na riba kama kuna suala na sababu maalum” alibainisha Mhe. Chande.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) alisema kuwa Serikali ilifuta utaratibu kwa walipakodi kulipa kodi kabla ya kuanza biashara ili kutoa nafasi ya kujiimarisha kibiashara.
Alisema hayo alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, aliyetaka kujua muda ambao Serikali itaondoa utaratibu wa biashara mpya kutakiwa kulipa kodi ya mapato kabla ya biashara kuanza.
Mhe. Chande alisema mwaka 2019/20 baada ya Serikali kufuta utaratibu huo walipakodi wote wanatakiwa kulipa kodi miezi sita (6) baada ya kufungua biashara na kuongeza kuwa utozaji wa kodi ya mapato hufanyika kulingana na mapato yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka husika.
Aidha, aliiagiza TRA kuendelea kufuata sheria, utaratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Mwisho.