Kaimu Mkurugenzi, Huduma kwa wateja wa TANESCO Martin Mwambene Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TANESCO mkoa wa Ilala Posta jijini Dar es Salaam leo kuelezea hali ya upatikanaji wa umeme karika siku zjazo.
Bw. Elihuruma Ngowi Meneja Mawasiliano wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO akiwa katika mkutano huo.
…………………………………
Mradi wa kituo cha Ubungo namba tatu chenye uwezo wa kuzalisha megawati 112 kinachozalisha umeme kwa gesi umekamilika huku Mradi wa Kinyerezi 1 Extension ambao utaingiza jumla ya megawati 185 katika gridi ya Taifa ukitarajiwa kukamilika hivi karibuni kutaimarisha zaidi upatikanaji wa huduma umeme nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi, Huduma kwa wateja wa TANESCO Martin Mwambene wakati akizungumzia kuhusu vyanzo mbadala vya uzalishaji wa umeme vilivyopunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini hali iliyotokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha athari nyingi ikiwemo upungufu wa vipindi vya mvua na kusababisha ukame.
Ameongeza kuwa umeme unaotokana na nguvu za jua mkoani Shinyanga na Kishapu unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2023 ukiingiza megawati 50 kati 150 hali itakayoboresha zaidi upatikanaji wa umeme kwa watanzania.
Katika kukabiliana na mabadiliko hayo na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa wananchi wote, kuanzia mwaka jana Shirika hilo lilianza mikakati ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mseto vya nishati.
“Tusingeanzisha mipango hii ya kutekeleza miradi hii pengine hali ya upatikanaji wa umeme ingekuwa mbaya zaidi tofauti na ilivyo sasa,”. Amesema Martin Mwambene
Mwambene ameongeza kuwa katika baadhi ya maeneo kadhaa kwa baadhi ya mikoa yataathirika katika nyakati tofauti na TANESCO itaendelea kuwataarifu wateja wake kadiri miradi hii itakapokuwa inaanza kuingiza umeme katika gridi.”
Shirika hilo linaendelea kuongeza vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu na tayari TANESCO imeingia makubaliano na Kampuni ya Madsar ya Abudhabi, Dubai na watashirikiana katika kuwezesha miradi mbalimbali ya umeme jadidifu utakaofikia megawati 2000.