CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimeunga mkono kauli ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ya kuiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kukamilisha haraka Barbara ya mchepuko katika eneo la Mlima Inyala Mkoani Mbeya kwa lengo la kudhibiti ajali zinazotokea katika eneo hilo.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Mweka Hazina wa TABOA Issa Nkya alisema agizo la Dk Mpango alilolitoa kuhusu eneo hilo ndiyo mwarobaini pekee wa kupunguza au kumaliza kabisa tatizo katika eneo hilo ambalo limekuwa chanzo cha ajali nyingi zinazopoteza maisha ya watu.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk Mpango kwa kuiona changamoto iliyopo katika eneo hilo kwani imekuwa chanzo cha vifo vingi vitokanavyo na ajali za barabarani ikiwemo iliyotokea jana na kuchukua uhai wa Mkurugenzi wa Igunga na Dereva wake” alisema Nkya ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Usalama Barabarani Taifa.
Amesema changamoto ya miundombinu katika eneo hilo ndiyo hasa kichocheo cha ajali na vifo na hakuna uhusiano na makosa ya Jeshi la Polisi katika suala la magari kufeli breki, hivyo hawapaswi kupewa lawama na kubadirishiwa vituo vya kazi badala ya patengenezwe kama ambavyo Makamu wa Rais ameagiza.
Awali September 12 Mwaka huu akiwa katika eneo hilo la Inyala, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alitoa agizo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kukamilisha haraka barabara ya mchepuko katika eneo la Mlima wa Inyala uliopo Kijiji cha Shamwengo ili kupunguza matukio ya ajali katika eneo hilo.
Mbali na hilo pia alitoa siku 10 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mbeya wamalize ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari katika eneo la Mlima wa Inyala mkoani Mbeya ili kukabili changamoto ya ajali mara kwa mara.
Dk Mpango alitoa maagizo hayo ikiwa ni siku chache tangu zilipotokea ajali mbili na kusababisha vifo vya watu wapatao 25 kabla ya hapo jana kutokea ajali nyingine ambayo imesababisha kifo cha Mkurugenzi wa Wilaya ya Igunga na dereva wake wakiwa njiani kutoka Mkoani Mbeya alipokuwa akishiriki mkutano wa ALAT.
Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.5 ni vyema ikajengwa haraka kwa kiwango cha lami kurahisisha upishanaji wa magari katika eneo hilo huku akimuagiza aliyekuwa kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Urich Matei kusmamia ukaguzi wa magari yanayopita katika eneo la mlima wa Inyala ili kuepusha madhara ya ajali zinazojitokeza kutokana na ubovu wa magari.
Dk Mpango alisema serikali inasikitishwa na madhara ya ajali yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka wahusika likiwemo Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao, kauli ambao TABOA kupitia Mweke Hazina wake huyo aliipongeza na kuitolea msisitizo kuwa ndiyo tiba ya ajali nchini.
Alisema wao kama TABOA wanathamini sana usalama wa maisha ya watu na mali zao hivyo wao kama wadau muhimu katika sekta ya usafirishaji wana wajibu wa msingi kuhakikisha suala la usalama linasimamiwa kikamilifu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango alipotembelea eneo la ajali juzi.