Mkurugenzi wa leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) Andrew Mkapa akizungumza wakati alipokuwa akifungua kikao kati ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) pamoja na Taasisi za Sekta za Umma ili kupata maoni na mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya leseni za Biashara ya mwaka 1972.
…………………………..
Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) pamoja na Taasisi za Sekta za Umma wamekutana ili kupata maoni na mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya leseni za Biashara ya mwaka 1972.
Akifungua kikao hicho leo Jumatano Septemba 14,2022 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) Andrew Mkapa amesema kupitia kikao hicho kutawezesha kupatikana mchango utakaofanikisha maboresho ama marekebisho ya Sheria ya leseni za Biashara , Sura 208 ambayo imeonekana kupitwa na wakati.
Aidha Andrew Mkapa amesema Sheria iliyopo kwa sasa haiendani na mazingira ya wakati huu ambapo imeonekana kuwepo na mikwamo kadhaa kutokana na Mabadiliko ya Teknolojia ya Ufanyaji Biashara huku akitolea mfano uwepo wa Biashara za Mitandao.
Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji , Viwanda na Biashara (WUVB ) Denis Mzamiru amesema kinachowasukuma kufanya maboresho na Marekebisho ya sheria hiyo ni pamoja na kuifanya Sheria kuendana na Mazingira ya Sasa ya Ufanyaji Biashara ikienda sambamba na uwepo wa urahisi na wepesi kwa wafanyabiashara kupata leseni za Biashara.
Kikao hicho cha Siku tatu pia kitawashirikisha wafanya biashara binafsi kupitia miavuli yao kimeandaliwa na Brela ikiwa ni agizo kutoka kwa Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji kutaka kuwepo kwa mchakato wa kuboresha sheria ikienda sanjari na kushirikishwa kwa wadu wanaoitumia sheria hiyo .
Picha mbalimbali zikonesha washiriki wa kikao hicho kutoa taasisi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya uzinduzi.