Na Englibert Kayombo – WAF, Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Isdor Mpango ameiagiza Wizara ya Afya kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kufanya tafiti ya ongezeko la ugonjwa wa Saratani katika Kanda ya Ziwa.
Dkt. Mpango amesema hayo kufuatia ongezeko kubwa la watu kutoka Kanda ya Ziwa wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Saratani huku pia akisema kuna tetesi zinazohusisha matumizi ya dawa za kuoshea maiti kutumika kuhifadhia samaki jambo linalopekea kuwa na idadi kubwa ya watu waaougua Saratani kutoka Kanda ya Ziwa.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema hayo mara baada ya kuzindua Jengo la Wodi ya Huduma za Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando lililojengwa kwa thamani ya Shilingi Bilioni 5.6.
“Kupitia fedha za UVIKO-19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 6.1 kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi naiagiza Wizara ya Afya kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kufanya tafiti kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kuhusu ongezeko la ugonjwa wa Saratani” amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango ameviagiza vyombo vya udhibiti na usalama kuchukua hatua za haraka na kufuatilia tetesi zinazohusisha matumizi ya dawa hizo na kuchukua hatua madhubuti.
Aidha Dkt. Mpango amewataka wananchi wanaohusika kufanya vitendo hivyo kuacha mara moja kwa kuwa kufanya hivyo ni kuangamiza wananchi kwa ugonjwa wa Saratani.