TAASISI isiyo ya kiserikali ya Tanzanite Support Organization (TSO) imezinduliwa leo kwa ajili ya kusaidia watoto yatima wanaofikisha miaka ya kuondoka katika vituo vya kulelea watoto yatima.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, leo Septemba 12, 2022 Mkurugenzi wa Tanzanite Support Organization(TSO), Bahati Chando amesema kuwa lazima jamii ijiulize watoto wanaotoka katika vituo hivyo waenda wapi kipindi wanapofikisha miaka 18 ya kuondoka katika vituo hivyo.
Amesema kuwa taasisi hiyo itakuwa inamulika ndoto za watoto hao ili waweze kujisimamia katika kujipatia kipato chao wenyewe pindi tuu wanapofikisha umri wa kuondoka katika Vituo vya kulelea watoto yatima.
Amesema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuwawezesha watoto waliopo katika Makao ya kulelea watoto yatima ili waweze kujitegemea.
Kwa Upande wa Afisa Ustawi wa Jamii, Neema Mwalubilo amesema taasisi hiyo imefunguliwa kwa wakati muafaka sasa watakuwa na pa kuwapeleka watoto waliofikisha miaka 18 ili kwenda kupata ujuzi mbalimbali ili waweze kujikwamua katika maisha yao.
“Tulipopata barua kutoka taasisi hii tulifurahi kama Ustawi wa jamii kwasababu taasisi hii imekuja kwa wakati uliosahihi, huyu mtoto atakapopata elimu kutoka taasisi hii ya Tanzaniate Support Organization huyu mtoto ataweza kujitegemea na kuanzisha familia yake.” Amesema Neema
Amesema kuwa Watoto wanaofikisha miaka 18 na kuendelea hawana haki ya kuoa wala kuolewa wakiwa kwenye makao, lakini wakitoka pale wanaweza kuoa na kuolewa kwani watakuwa wanajitegemea.
“Taasisi hii imekuja kutusaidia katika jambo ambalo tulikuwa tunahangaika nalo kwa muda mrefu.”
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa TPDC, Idris Hashim amesema amewashukuru TSO kwa kuwa na wazo la kuwasaidia watoto wanaofikisha miaka 18 na kuendelea ili kuwapa ujunzi ambao utawasaidia katika kujitegemea wao wenyewe.
Kwa upande wa wadau waliounga mkono juhudi za uanzishwaji wa taasisi hiyo wamesema taasisi hiyo isimamie malengo yake ili iweze kuwafikia vijana wengi zaidi. Pia amewaomba wadau waweze kujitoa kwaajili ya kuwapa elimu na ujuzi katika kuwatimizia malengo vijana hao wataokuwa wametoka kwenye makao ya kulelewa.